1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitunishia misuli Korea kaskazini

Halima Nyanza29 Juni 2011

Marekani jana iliweza kudhihirisha ubabe wake kwa Korea Kaskazini, baada ya kuinyuka mabao mawili kwa bila, katika mchezo uliochezwa katika mji wa Dresden hapa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/11l6e
Wamarekani wakishangilia ushindiPicha: dapd

Lauren Cheney wa Marekani ndiye aliyeanza kuliona lango la wa Korea Kaskazini katika dakika ya 54, toka kuanza kwa mchezo. Na katika dakika 76, Rachel Buehler wa Marekani, alilizamisha kabisa Jahazi la Korea kaskazini kwa kuongezea timu yake bao la pili.

Mabao yote hayo mawili yaliyowafanya Marekani kutoka kifua mbele katika mchezo wa jana, yalipatikana katika kipindi cha pili.

Frauenfußball WM 2011 USA vs Nordkorea Pia Sundhage
Kicha wa Marekani, Pia SundhagePicha: picture alliance/dpa

Akizungumzia matokeo hayo kocha wa Timu ya soka ya wanawake wa Marekani, Pia Sundhage alisema wamefanya kazi nzuri, kutokana na kwamba ni vizuri kupata matokeo kama hayo, kwa vile itakuwa rahisi kwao kuweza kusonga mbele.

Kwa upande wake, kocha wa timu ya Soka ya wanawake ya Korea kaskazini , ambao ni mabingwa mara tatu  barani Asia, Kim Kwang Min amesema mchezo wa jana haukuwa mzuri kwao, kutokana na wachezaji wengi kucheza wakiwa majeruhi, baada ya kupata ajali katika kambi yao ya mazoezi mjini Pyongyang, June 8, ambapo baadhi ya wachezaji walipelekwa hospitali.

Ameongezea kusema kuwa mpaka sasa baadhi ya wachezaji bado hawajawa na afya nzuri kwa ajili ya mchezo.

Frauen Fußball WM 2011 Schweden vs Kolumbien
Hekaheka goliniPicha: dapd

Na katika pambano jingine hapo jana, Sweden, iliweza kuibuka kidedea baada ya kuibwaga Colombia bao moja kwa bila, katika mchezo uliochezwa katika mji wa Leverkusen hapa Ujerumani.

Matokeo hayo ya jana kwa timu zote nne zilizojitupa uwanjani, zimefanya Marekani, mabingwa mara mbili, kuongoza kundi C, ikifuatiwa na Sweden.

Na leo basi msikilizaji wawakilishi wa Afrika, Guinea ya Ikweta itajitupa uwanjani Kumenyana na Norway huku Brazili wakivaana na Australia.

Wawakilishi wengine wa Afrika, Nigeria, watashuka dimbani hapo kesho kupambana na wenyeji na mapingwa watetezi Ujerumani, timu ambayo mmoja wa makocha wake Ulrike Ballweg anasema kwamba wamejipanga vizuri kuonesha kabumbu safi.

Anasema bila ya shaka yoyote wanataka kucheza vizuri zaidi. Kama ilivyokwishaonekana, wameonesha kiwango kizuri, mchezo wao wa pasi na staili ya kukishirikisha kikosi kizima.

Lakini hata hivyo kocha wa Ujerumani Ulrike Ballweg hakuonesha kuidharau timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Nigeria.

Amesema kimazoezi Wanigeria ni wazuri sana. Wana kasi sana uwanjani, wanacheza wakiwa wametulia tangu mwanzo. Pia wameona kuwa wanaitumia kila fursa inayopatikana, ama kwa kasi au kwa kikosi kizima kuja mbele."

Leo ni siku ya nne, toka michuano ya kombe la dunia la soka la wanawake mwaka 2011, ilipoanza hapa Ujerumani.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, Reuters, FIFA.com)