1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitishia vikwazo zaidi Urusi

Admin.WagnerD11 Aprili 2014

Rais wa Marekani Barack Obama ametishia kuiwekea Urusi vikwazo zaidi, iwapo itazidi kuchochea mgogoro juu ya Ukraine, huku muda wa mwisho uliyotolewa na serikali mjini Kiev kwa wanaopenda kujitenga ukiisha Ijumaa.

https://p.dw.com/p/1BgMo
Waandamanaji mjini Donetsk.
Waandamanaji mjini Donetsk.Picha: picture-alliance/dpa

Taarifa ya ikulu ya White House ilisema baada ya rais Obama kuzungumza na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa njia ya simu siku ya Alhamisi, kuwa Obama alisisitiza nchi yake na Umoja wa Ulaya pamoja na washirika wengine wa kimataifa laazima wawe tayari kukabiliana na ongezeko la chokochoko za Urusi kwa kuiwekea vikwazo zaidi.

Marekani pia ilitoa onyo kwa Urusi wakati wa mikutano ya benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF mjini Washington, huku kukiwa na wasiwasi kuwa mgogoro wa Ukraine unaozidi kuchacha unaweza kuuathiri uchumi wa dunia.

Rais wa Urusi Vladmir Putin.
Rais wa Urusi Vladmir Putin.Picha: Sergei Chirikov/AFP/Getty Images

Waziri wa fedha wa Marekani Jack Lew alimuambia mwenzake wa Urusi Anton Siluanov kwamba pamoja na vikwazo vilivyofuatia hatua ya Urusi kuliteka eneo la Crimea mwezi uliyopita, Marekani iko tayari kuiwekea Urusi vikwazo zaidi ikiwa itaendelea kuchochea hali mbaya nchini Ukraine.

Serikali yahangaika kuzuwia vurugu

Katika jitihada za kuzuia mgawanyiko wa taifa hilo, viongozi wa Ukraine waliahidi siku ya Alhamisi kutoa msamaha kwa wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi, wanaoyakalia majengo ya serikali katika miji ya mashariki, ikiwa wataweka chini silaha zao na kusitisha uzingiraji wa majengo hayo uliyodumu kwa siku nne sasa.

Waziri mkuu wa muda wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk aliekuwa mjini Donestk, aliwambia viongozi wa maeneo hayo kuwa yuko tayari kuhurusu majimbo kuwa na mamlaka zaidi. Yatsenyuk, aliuambia mkutano wa viongozi hao, ambao haukawahusisha wawakilishi wa makundi ya wanaotaka kujitenga, kwamba mamlaka zaidi yanapaswa kutolewa kwa viongozi wa majimbo.

Rais wa muda wa Ukraine Oleksander Turchinov, alieko madarakani tangu kiongozi anaegemea upande wa Urusi Viktor Yanukovych alipoondolewa madarakani mwezi Februari, aliwaambia wabunge kuwa mgogoro wa kujitenga kwa baadhi ya maeneo unaweza kutatuliwa kwa njia za amani, ikiwa watu wenye kupenda kujitenga wataweka chini salaha na kuyaachia majengo ya serikali.

Picha za Setilait za NATO zikionyesha wanajeshi wa Urusi walioko mpakani mwa Ukraine.
Picha za Setilait za NATO zikionyesha wanajeshi wa Urusi walioko mpakani mwa Ukraine.Picha: DigitalGlobe/SHAPE/dpa

Ugavi wa gesi kwa Ulaya hatarini

Mapema watu wanaotaka kujitenga kwa jimbo la Donetsk walitangaza kuunda Jamhuri yao na kumtolea wito rais Vladmir Putin kuviagiza vikozi vya Urusi kuingia katika eneo hilo lenye viwanda nchini Ukraine. Katika kuchochea zaidi mgogoro huo, Urusi iliuonya Umoja wa Ulaya Alhamisi kuwa ugavi wake wa nishati ya gesi unaweza kuathirika ikiwa umoja huo hautaisaidia Ukraine kulipa madeni yake.

Onyo hilo la rais Putin kuhusu ugavi wa gesi, ambayo ni muhimu sana kwa uhai wa kiuchumi wa mataifa ya Ulaya, limekuja wakati uhusiano baina ya Urusi na mataifa ya magharibi uko katika kiwango cha chini kabisaa tangu kumaliza kwa vita baridi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe,ape.
Mhariri: Saum Yusuf