1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka UN kutumia nguvu kuwalinda raia

12 Mei 2016

Marekani imeahidi kuunga mkono mpango wa kanuni kadhaa zinazowapa mamlaka wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na polisi kutumia nguvu ili kuwalinda raia katika migogoro ya kivita.

https://p.dw.com/p/1ImAS
Symbolbild UN Blauhelme
Picha: MENAHEM KAHANA/AFP/Getty Images

Mpango huo umeungwa mkono na Rwanda na Uholanzi. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power ametoa tangazo hilo katika mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ulioangazia wajibu wa kuwalinda raia wanaokumbwa na machafuko, akisema kuwa Marekani “inajivunia” kujiunga na mataifa mengine 28 yaliyosaini mpango huo unaojulikana kana Kanuni za Kigali.

Walinda amani kutoka nchi 29 katika operesheni zilizoidhnishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwalinda raia sasa wanaruhusiwa kuchukua “hatua ya moja kwa moja ya kijeshi dhidi ya makundi yenye silaha yenye nia ya wazi ya kuwadhuru raia” – na makamanda wao wanaweza kuamuru matumizi ya nguvu “katika hali ya dharura” bila kushauriana na wakuu wao.

Power amesema Kanuni za Kigali zimetayarishwa kuhakikisha kuwa raia hawatelekezwi tena na jamii ya kimataifa, akirejelea namna walinda amani wa Umoja wa Mataifa walivyoondoka Rwanda kabla ya mauaji ya halaiki ya mwaka wa 1994 na Srebrenica kabla ya mauaji ya kinyama ya 1995.

Simon Adams, mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Wajibu wa Kulinda, anasema 10 kati ya operesheni 16 za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, ikiwemo asilimia 97 ya wanajeshi 105,000 na polisi wanaohudumu katika operesheni hizo, wana wajibu wa Baraza la Usalama kuwalinda raia.

Karte UN peacekeeping troop and police contributors ENG

Hata hivyo, licha ya kuwapo kwa operesheni za kulinda amani Umoja wa Mataifa unaendelea kupambana kuwalinda raia dhidi ya makosa mengi ya kikatili katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, Sudan na Sudan Kusini. Anaongeza Adams.

Power alisema nchi 29 ambazo zimeidhinisha Kanuni za Kigali zinajumuisha zaidi ya wanajeshi 40,000 wa Umoja wa Mataifa na polisi, ikiwa ni zaidi ya thuluthi moja ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa ndio mchangiaji mkubwa wa kifedha kwa operesheni za kulinda amani za umoja huo lakini una wanajeshi wachache mno wanaotumwa katika operesheni zake.

Rwanda, Uholanzi na Marekani ziliuanzisha mpango huo wa msingi ambao uliidhinishwa katika mkutano wa ngazi ya juu mnamo Mei 2015 mjini Kigali na mataifa makuu 30 yanayochangia wanajeshi na polisi kwa operesheni za Umoja wa Mataifa, wachangiaji kumi wakuu wa kifedha namataifa mengine.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uholanzi Bert Koenders aliumbia mkutano huo kuwa watu na jamii zilizoko chini ya kitisho, bila mahali pa kwenda, zinapaswa kujua kuwa Umoja wa Mataifa utafanya kila liwezekanalo ndani ya uwezo wake kuwapa ulinzi.

Balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa Eugine-Richard Gasana alisema kanuni hizo zinaleta operesheni za kulinda amani “katika karne ya 21”. Amesema zaidi ya wanajeshi 6,000 wa Rwanda katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa wamepewa mafunzo ya kuzingatia kanuni hizo na “wamejiandaa kutumia nguvu ikiwa watahitajika” kwa ajili ya kuwalinda raia.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Iddi Sessanga