1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaishtaki BP, kwa uvujaji wa mafuta katika Ghuba ya Mexico

16 Desemba 2010

Serikali ya Marekani inataka BP na kampuni zingine 8 kuilipa fidia kwa hasara serikali hiyo ilipata kusimamisha uvujaji wa mafuta.

https://p.dw.com/p/QcrX
Kampuni ya mafuta ya BP yashtakiwaPicha: BP

Serikali ya Marekani kwa mara ya kwanza jana iliiwasilisha ombi la kuishtaki kampuni kubwa ya mafuta BP pamoja na kampuni zingine nane, kuilipa fidia ya mabilioni ya dola kwa uharibifu kutokana na kuvuja kwa mafuta katika Ghuba ya Mexico. Umwagikaji huo wa mafuta ndio ilikuwa tukio baya kabisa katika historia ya Marekani.

Ölpest USA Rettungsversuch BP
Mabilioni ya lita ya mafuta yalimwagikaPicha: AP

Ombi hilo liliwasilishwa na Wizara ya sheria katika mahakma moja mjini New Orleans. Maelfu ya watu wengine ikiwemo wafanyabishara pia wameishtaki kampuni hiyo kubwa ya mafuta katika mji huo huo.

Kulingana na mwanasheria Mkuu wa Marekani Eric Holder kampuni hiyo ya mafuta ya BP na kampuni hizo nane zinalaumiwa kwa kukiuka sheria za usalama, iliosababisha  kutokea kwa ajali hiyo- pale kisima cha Deepwater Horizon kilio chini ya bahari kilipolipuka Aprili 20. Matokeo yake ilikuwa ni kuvuja kwa mabilioni ya lita za mafuta yaliyosambaa kote katika Ghuba hiyo ya Mexico.

Ölpest USA Golf von Mexiko BP Obama
Fidia hiyo ni mabilioni ya dolaPicha: AP

Holder alisema wana lenga kuthibitisha kuwa walalamikiwa katika kesi hiyo wana jukumu chini ya kifungu cha sheria kuhusiana na uharibifu wa mazingira kuifidia serikali kwa gharama zote za kusimamisha umwagikaji huo, hasara ya kiuchumi iliopatikana pamoja na uchafuzi wa mazingira.

Mwanasheria huyo mkuu aliongeza kuwa serikali ya Marekani katika kesi hiyo pia inataka kupiga marufuku uchimbaji wa mafuta chini ya bahari ambao haujaidhinishwa- hii ikiwa ni chini ya kifungo cha sheria kinachotaka kuwepo kwa maji safi.

Katika malalamiko yao serikali ya Marekani ilisema BP hawakuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kisima hicho ni salama, na wala hawakutumia teknologia ya kisasa ya kuchunguza shughuli katika kisima hicho na kwamba vifaa vyake vya usalama vilikuwa na matatizo.

Katika taarifa yake BP ilisema itajibu madai hayo ya Marekani katika wakati ufaao na kwamba bado wataendelea kushirikiana na uchunguzi wote unaondeshwa kuhusiana na umwagikaji huo wa mafuta.

BP, kampuni ya tatu kubwa ya mafuta duniani imejitetea kuhusiana na namna ilivyokabiliana na janga hilo, ikiwemo kuuza mali zake katika maeneo mbali mbali duniani ili kukusanya kiasi ya dola bilioni 30 kuwalipa fidia waathiriwa na kusimamisha umwagikaji huo wa mafuta.

Mwandishi: Munira Muhammad/afpe

Mhariri: Aboubakary Liongo