1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

USA Nordkorea

Charo Josephat9 Juni 2009

Hali ya wasiwasi kati ya Marekani na Korea Kaskazini yazidi

https://p.dw.com/p/I65m
Laura Ling (kulia) na Euna LeePicha: AP

Takriban miezi mitatu tangu walipokamatwa nchini Korea Kaskazini, waandishi wawili wa habari wa Korea Kaskazini wamehukumiwa kifungo cha miaka 12 katika kambi ya kazi ngumu. Mahakama kuu ya mjini Pyongyang ilifikia uamuzi huo baada ya kuisikiliza kesi hiyo kwa siku kadhaa. Wamarekani hao inadaiwa waliingia nchini Korea Kaskazini bila kibali na kufanya ukatili dhidi ya wananchi wa Korea Kaskazini. Wadadisi wanasema Korea Kaskazini inawatumia waandishi hao wa habari kama chambo kuishinikiza Marekani ifanye mazungumzo na utawala wa Pyongyang.

Hukumu dhidi ya waandishi wawili wa habari wa Marekani, Laura Ling na Euna Lee wafanyakazi wa televisheni ya Current, imezidisha hali ya wasiwasi ambayo imekuwepo kati ya Korea Kaskazini na utawala wa mjini Washington. Rais wa Marekani Barack Obama ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu maripota hao wa televisheni. Msemaji wa ikulu ya Marekani, Robert Gibbs, amesema kila juhudi zitafanywa kuhakikisha waandishi hao wa habari wanaachiwa huru. Gibbs aidha amesema hatima ya waandishi hao haipaswi kuhusishwa na mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Jamaa wa Laura Ling na Euna Lee wameitolea mwito Korea Kaskazini iwaachie huru warejee nyumbani kwa kuwa miezi mitatu waliyozuiliwa huku wakiwa na mawasiliano machache na familia zao inatosha. Mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo Amnesty International, yameishutumu Korea Kaskazini kwa jinsi ilivyoishughulikia kesi ya waandishi hao. Maandamano yamefanywa katika miji mikubwa ya Marekani kuishinikiza Korea Kaskazini iwaachie Laura na Euna.

Waziri wa mashauri ya kigeni ya Marekani Hillary Clinton amesema juhudi zimeanza kuchukuliwa kujaribu kuwaokoa waandishi hao.

"Tunafanya kila juhudi na kutumia kila njia inayowezekana kuhakikisha wanaachiwa huru. Na kwa mara nyingine tunaihimiza Korea Kaskazini iidhinishe kuachiwa kwao mara moja kwa sababu za kibinadamu."

Hillary Rodham Clinton USA Wahlen
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Hillary Rodham ClintonPicha: AP Photo/M. Spencer Green

Marekani inajadili uwezekano wa kumtuma mjumbe wake maalumu nchini Korea Kaskazini kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo ili waandishi hao warejeshwe Marekani. Wizara ya mambo ya kigeni imesema haijafuta uwezekano wa makamu wa rais wa zamani wa marekani, Al Gore kwenda Korea Kaskazini. Laura na Euna walikamatwa karibu na mpaka kati ya China na Korea Kaskazini wakati walipokuwa wakitayarisha ripoti kwa ajili ya kampuni iliyoasisiwa na Al Gore.

Hata balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Bill Richardson, ni miongoni mwa watu wanaofikiriwa kuchukua jukumu hilo la kidiplomasia. Mwenye amesema wakati alipohojiwa na televisheni ya CNN kwamba atakuwa tayari kujihusisha na swala hilo. Richardson alifaulu kuwaokoa Wamarekani wawili kutoka Korea Kaskazini katika miaka ya 1990.

Ukiacha kando swala la waandishi wa habari, waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, anashinikiza kwamba Korea Kaskazini irejeshwe katika orodha ya mataifa yanayodhamini ugaidi. Rais wa zamani wa Marekani, George W Bush aliiondoa Korea Kaskazini kutoka kwa orodha hiyo mnamo mwaka jana.

Uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini unakabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na matukio ya hivi karibuni ambapo serikali ya Pyongyang ilifyetua roketi lake na kufanya majaribio ya makombora yake ya masafa marefu. Kwa mujibu wa taarifa za magazeti serikali ya Marekani inachunguza meli za Korea Kaskazini ambazo huenda zinasafirisha silaha na kuzisimamisha ili zipekuliwe. Korea Kaskazini imetishia kuchukua hatua za kijeshi iwapo Marekani itafanya hivyo.

Mwandishi :Ziegler Albrecht/ZR/Josephat Charo

Mhariri:M.Abdul-Rahman