1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaadhimisha miaka 8 ya vita Afghanistan.

7 Oktoba 2009

Marekani bado wanajaribu kutafuta mkakati wa kushinda vita Afghanistan, miaka minane tangu rais Bush kuanzisha vita hivyo.

https://p.dw.com/p/K0iG
Rais Barack Obama anakabiliwa na uamuzi mkubwa, Afghanistan.Picha: AP
USA Afghanistan Dänemark Treffen Barack Obama und General Stanley McChrystal Flughafen Kopenhagen
Rais Barack Obama akutana na Gen. Stanley McChrystal, Kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani, Afghanistan.Picha: AP

Rais Barack Obama leo atakutana na timu yake ya usalama wa kitaifa, kubadilishana mawazo, katika jitihada za kutafuta mkakati mpya wa kushinda vita nchini Afghanistan, katika siku ambayo Marekani inaadhimisha miaka minane tangu majeshi yake kuivamia Afghanistan kuwaondoa madarakani Wataliban. Wanajeshi wa Marekani bado wanajaribu kuwaangamiza wapiganaji wa Kitaliban miaka minane tangu rais George Bush alipotangaza vita dhidi ya Wataliban baada ya mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani.

Iwapo kuna wakati rais Barack Obama anahitaji kufanya maamuzi ya haraka ni sasa, kuhusiana na Afghanistan. Obama leo atakutana na timu yake ya usalama wa kitaifa kuona ni mbinu ipi wataitumia kufanikiwa nchini Afghanistan, katika vita vya miaka minane sasa ambavyo vimewaua kiasi cha wanajeshi 800 wa Marekani, na sasa pia vimewachosha Wamarekani.

Vita hivyo vilivyoanzishwa baada ya mashambulizi ya Septemba 11, kuwaondoa madarakani Wataliban na kuwaangamiza Al-Qaeda waliokuwa na ngome yao Afghanistan, sasa vimechukua muda mrefu kinyume na ilivyotarajiwa, na hakuna dalili ya kwamba vitamalizika hivi karibuni.

Jana Rais Obama alikaa mezani na viongozi wa baraza la wawakilishi na viongozi wa baraza la Senate kutoka vyama vya Demokrats na Republicans kutafuta mchango wao kuhusiana na hali nchini Afghanistan. Na hasa kuhusiana na swala la kuwatuma wanajeshi wengine zaidi nchini Afghanistan.

Obama anajaribu kutafuta mchango wa kila upande kabla ya kufanya maamuzi. Mkutano wa jana na viongozi hao, hata hivyo haukumaliza tofauti baina ya vyama hivyo viwili.

Republicans wanasema, Obama hana muda wa kupoteza, kwani anahitaji kutekeleza pendekezo la Kamanda mkuu wa Majeshi ya Marekani Afghanistan, Generali Stanley McChrystal ambaye ameomba wanajeshi wengine, 40,000 kupelekwa nchini humo.

Afghanistan Treffen in Helmand Soldaten und Bevölkerung
Wanajeshi wa Marekani wafanya mkutano na raia wa Afghanistan.Picha: AP

Republicans wanasema iwapo Obama hatafanya hivyo basi atakuwa anahatarisha usalama wa Marekani na kutoa mwanya wa Marekani kushindwa Afghanistan.

Marekani tayri ina wanajeshi 68,000 Afghanistan na Demokrats wanapinga wazo la idadi hii kuongezwa wakisema Wamerakni tayari wamechoshwa na vita hivyo na huenda kuongezwa kwa wanajeshi Afghanistan kukamponza rais Obama aliyeingia madarakani kwa kauli mbiu ya kumaliza vita.

Leo atakapokutana na washauri wake wakuu akiwemo makamu wa rais Joe Biden, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton na waziri wa ulinzi Robert Gates, Obama atakuwa aanatilia maanani misimamo na mawazo ya kila pande aliyopata hadi kufikia sasa.

Iwapo Republicans watasalia na msimamo wao na Demokrats na msimamo wao- sasa itabidi Obama kuamua yeye binafsi upi utakuwa mwelekeo Afghanistan- na jinsi mambo yalivyo inaonekana huu ndio uamuzi aidha utauponza urais wake au utakuwa uamuzi utakaomzidishia ushawishi na haiba zaidi.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman