1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Ujerumani zapenya Baraza la Haki za Binaadamu

14 Novemba 2012

Marekani na Ujerumani zimejishindia viti katika Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa katika mchuano mkali wa kundi la mataifa ya magharibi wakati Kenya imekuwa mwanachama kwa kupitia kundi la Afrika.

https://p.dw.com/p/16hiw
Baraza la Haki za Binaadamu
Baraza la Haki za BinaadamuPicha: picture-alliance/dpa

Kufuatia ushindi huo Marekani imeahidi kukomesha mapungufu katika baraza hilo wakati Ujerumani ikisema kwamba msimamo wake utakuwa ule wa maafikiano.Marekani ni mojawapo ya nchi 18 kujishindia nafasi katika baraza hilo lenye nchi wanachama 47 kuanzia Januari Mosi mwakani.Lakini makundi ya kutetea haki za binaadamu yameshutumu uchaguzi wa kuwania viti vya baraza hilo uliofanyika katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa sababu ni mataifa ya magharibi tu yaliokuwa na uchaguzi wa wazi kugombania nafasi zao tatu kutoka kundi la mataifa hayo.

Venezuela na Pakistan ambazo rekodi zao za haki za binaadamu zimekuwa zikishutumiwa na wanaharakati na serikali zimejipatia kura zaidi kuliko hata Marekani,Ujerumani na Ireland ambazo zimechaguliwa kupitia kundi la mataifa ya magharibi.Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hilary Clinton amesema uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkubwa ambapo baadhi ya wanadiplomasia walitabiri kwamba Marekani ilikuwa katika hatari ya kushindwa katika uchaguzi huo wa kuwania kuchaguliwa tena kwenye baraza hilo kwa sababu iliingia katika dakika za mwisho.Lakini Clinton na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice ambaye anatajwa kwamba anaweza kuwa waziri mpya wa mambo ya nchi za nje wa Marekani wamesema serikali ya Marekani itaendeleza jitihada la kulifanyia mageuzi baraza hilo lenye makao yake mjini Geneva.

Clinton amesema katika taarifa kwamba wakati mengi bado yanahitajika kufanywa na baraza hilo hasa katika kukomesha mwelekeo wa baraza hilo kuiandama mno Israel,Marekani iko tayari kushirikiana na nchi nyengine wanachama wa baraza hilo kuendelea kushughulikia masuala ya haki za binaadamu na kuhakikisha kwamba baraza hilo linatimiza kikamilifu ahadi yake.Marekani ilikuwa imelisusia Baraza hilo la Haki za Binaadamu hadi hapo mwaka 2009 wakati utawala wa Rais Barack Obama ulipobadilisha sera ya Marekani na kugombania kiti kwenye baraza hilo katika juhudi za kulifanyia mageuzi wakati nchi hiyo ikiwa ndani ya baraza lenyewe.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton.Picha: dapd

Ujerumani taifa jengine kubwa lililojipatia kiti kwenye barara hilo limesema msimamo wake utakuwa ule wa maafikiano.Balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa Peter Witting amesema watakemea kwa sauti kubwa pale patakapokuwepo ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu na kukumbusha kwamba baraza hilo sio mahala pa kutowa madai holela. Balozi huyo amesema wangelipendelea kujenga mawasiliano na kushajiisha ushirikiano.Mataifa matano yaliwania viti vya kundi la mataifa ya magharibi ambapo Ugiriki na Sweden zilishindwa.Makundi mengine yote ya kanda yalifanya mipango kabla kuhakikisha kwamba nchi zinazoteuliwa zinalingana na viti vya kanda husika.Mashirika ya haki za binaadamu yameshutumu kupikwa kabla kwa mipango hiyo kuwa ni doa kwa sifa ya baraza hilo.

Kenya,Ivory Coast,Ethiopia,Gabon na Sierra Leone zinajiunga na baraza hilo kwa ajili ya Afrika. Japani,Kazakhstan,Pakistan,Korea Kusini na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya Asia.Brazil na Venezuela kwa ajili ya Amerika Kusini na Karibian wakati Estonia na Montenegro zitajiunga kwa ajili ya Ulaya mashariki.Shirika la haki za binaadamu lenye makao yake mjini Washington Marekani la Freedom House limesema kwamba nchi saba zilizojipatia viti katika baraza hilo yaani Ivory Coast,Ethiopia,Gabon, Kazakhstan,Pakistan,Umoja wa Falme za Kiarabu na Venezuela hazistahiki kuwa wanachama wa baraza hilo ambapo wanachama wanatakiwa wawe wenye kushikilia viwango vya juu kabisa vya kuheshimu haki za binaadamu.Hata nchi nyengine tatu wanachama wapya wa baraza hilo za Brazil,Kenya na Sierra Leone sifa zake zinatajwa kuwa ni za kutiliwa mashaka.

Bendera ya taifa la Kenya.
Bendera ya taifa la Kenya.Picha: picture-alliance/dpa

Mapema mwaka huu Sudan ilitangaza mipango ya ya kugombania kiti katika Baraza hilo la Haki za Binaadamu lakini ilijitowa baada ya kushutumiwa na mashirika ya haki za binaadamu.Syria pia ilijaribu kuwania kiti katika baraza hilo hapo mwaka jana lakini ilijitoa kutokana na shinikizo kutoka kwa mataifa ya magharibi na ya Kiarabu.Watetezi wa haki za binaadamu walifanikiwa katika kampeni kama hizo huko nyuma kwa kuzizuwiya kujiunga na baraza hilo nchi kama vile Belarus,Sri Lanka,Azerbaijan na Iran.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman