1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani - September 11

Mohamed Dahman11 Septemba 2010

Marekani inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 9 ya shambulio la kigaidi la Septemba 11.

https://p.dw.com/p/P9nJ
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP


Rais wa Marekani Barack Obama amewakumbusha wananchi wa Marekani juu ya umoja walio nao nchini humo kufuatia kumbukumbu ya miaka 9 ya shambulio la Septemba 11 na kuwaomba wazingatie lile linalowaunganisha na sio yale yanayowatenganisha.

Rais Obama amesema hayo wakati Marekani inajitayarisha kwa kumbukumbu ya shambulio hilo la Septemba 11, huku kukiwa na mgongano kati ya jamii za dini tofauti nchini humo. Mpango wa kujenga msikiti katika eneo la Manhattan sio mbali na eneo la World Trade Center lilioshambuliwa na mashambulizi hayo ya kigaidi ,umezua mjadala mkali nchini humo.Pia mkusanyiko wa kundi dogo la waumini wa dini ya Kikristo katika jimbo la Florida linaloongozwa na mchungaji mwenye itikadi kali za dini hiyo,Terry Jones, ulipanga kuchoma kitabu kitukufu cha dini ya Kiislamu,Quran katika kuadhimisha siku hii.Pendekezo ambalo limeshutumiwa na viongozi wengi wakiwemo wa jeshi,dini ,na siasa.

Ground Zero in New York 2010 NO-Flash
Ujenzi upya unaendelea katika eneo la World Trade Center mjini New York.Picha: AP

Pendekezo hilo la kuichoma Quran limeahirishwa.

Rais Obama anatarajiwa kuadhimisha kumbukumbu hiyo kwa hotuba na kuweka shada la maua katika eneo ambalo ndege mojawapo iliyotekwa nyara na magaidi ililijibamiza na jengo la wizara ya ulinzi, Pentagon nje ya mji mkuu wa Washington.Makamu wake Joe Biden, anatarajiwa kuhudhuria misa ya maombi mjini New York ambapo ndege mbili zilijibamiza na majengo mawili ya World Trade Center.

Mwandishi Maryam Abdalla
Mhariri:Dahman Mohammed