1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi zakubaliana kusitisha mapigano Syria

Sekione Kitojo
8 Julai 2017

Mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la mataifa yaliyoendelea duniani na yanayoinukia kiuchumi, G20 unaingia siku ya pili na ya mwisho leo baada ya kuanza jana mjini Hamburg, Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2gBTr
Deutschland Hamburg - G20 - Donald Trump und Vladimir Putin
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Rais wa Marekani Donald Trump na  rais Vladimir Putin  wa  Urusi jana  Ijumaa  walikubaliana  mpango  wa  kusitisha  mapigano  katika maeneo  ya  kusini  na  magharibi  mwa  Syria , ikiwa  ni  jaribio  la hivi  karibuni  kabisa  la  kusitisha  umwagikaji  wa  damu  katika  nchi hiyo  iliyoharibiwa  kwa  vita.

Makubaliano  hayo  yataanza  kutekelezwa  mchana  saa  za  Syria siku  ya  Jumapili, wanadiplomasia  wa  ngazi  ya  juu  wa  Urusi  na Marekani  wamesema  wataka  wakitangaza  makubaliano  hayo yaliyofikiwa  na  viongozi  wao  pembezoni  mwa  mkutano  wa  kilele wa  kundi  la  mataifa  yaliyoendelea  na  yanyoinukia  kiuchumi G20 nchini  Ujerumani.

G20 Gipfel in Hamburg | Putin & Trump
Rais Putin wa Urusi (kulia) na Donald Trump wa Marekani (Kulia)Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

"Ni mafanikio yetu ya  kwanza ," amesema  waziri  wa  mambo ya kigeni  wa  Marekani Rex Tillerson akizungumzia  ushirikiano  baina ya  Ikulu  ya  Marekani  White House  na  Kremlin.

Shirika  linaloangalia  haki  za  binadamu  nchini  Syria  limesema makubaliano  hayo  ya  kusitisha  mapigano  yalikuwa  yanatarajiwa kujumuisha  miji  ya  Daraa, Sweida  na  Queitra.

Rex Tillerson Australien
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex TillersonPicha: Reuters/J.Reed

Limesema  katika  taarifa  iliyotolewa  jana Ijumaa  kwamba makubaliano  hayo  yatashuhudia  kuondolewa  kwa  majeshi  ya serikali  ya  Syria  kutoka  katika  mstari  wa  mbele  na  kurejea katika  makambi.

Wakimbizi kurejea nyumbani 

Eneo  hilo litatayarishwa  kuwapokea wakimbizi  wa  Syria  kutoka Jordan. Pia  ina  maana  ya  kuruhusu misaada  wa  kiutu  kuwasili katika  eneo  hilo.

Vita  nchini  Syria , ambayo  hivi  sasa  vimo katika  mwaka  wa saba , vimeyaingiza  mataifa  makubwa  duniani  ikiwa  ni  pamoja na  Marekani  na  Urusi.

Wakati  huo  huo  polisi  walisumbuka  kuweza  kuwadhibiti waandamanaji  waliokuwa  wakifanya  ghasia  wakati  maelfu  ya waandamanaji  wenye  msimamo  mkali  wa  mrengo  wa  kushoto walifanya  fujo  katika  mji  wa  Hamburg , ambako  Ujerumani  ni mwenyeji  wa  mkutano  wa  G20.

Deutschland Hamburg - G20 Proteste
Waandamanaji wakiandamwa na polisi wa Ujerumani mjini Hamburg Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schrader

Kansela Angela  Merkel  alishutumu ghasia  hizo na  kusema ,"hazikubaliki," akiongeza  kwamba  alikuwa  "anatambua maandamano  ya  amani" lakini  maandamano  ya  ghasia yanahatarisha  maisha  ya  watu."

Mkutano wa G20 ulianza  rasmi  jana  Ijumaa  na  uliandamana  na maandamano  ya  ghasia  yaliyofanywa  na  wanaharakati  wa mrengo  wa  kushoto tangu  ulipoanza.

Mapema  jana  waandamanaji  walilazimisha  rais  wa  Marekani Donald Trump  kubadilisha  njia  kuelekea  katika  mkutano  huo  wa kilele, na  mkewe Melania , hakuweza  kushiriki  katika  mpango wa mkutano  wa  wake  wa  marais kwasababu  polisi  ilisema  ilikuwa  si salama kwake  kuondoka  katika  nyumba  alipofikizia.

Deutschland Hamburg - G20 Proteste
Ghasia za waandamanaji na polisi wakipambana kutuliza ghasiaPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schrader

Polisi  pia  walisema  waandamanaji 20 walishambulia  walinzi wa usalama  katika  hoteli  ya  Park Hyatt  mjini  Hamburg , ambayo amefikzia  rais  wa  Urusi Vladimir Putin , Moon Jae In wa  korea kusini  na  waziri  mkuu  wa  Australia  Malcom Turnbull.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / dpae

Mhariri: Josephat Charo