1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

170309 Guantanamo EU

Aboubakary Jumaa Liongo/ZPR17 Machi 2009

Marekani na Umoja wa Ulaya zimeanza mazungumzo yao ya mwanzo juu ya majaaliwa ya mahabusu wa gereza la Guantamo nchini Cuba.

https://p.dw.com/p/HEGu
Mahabusu katika gereza la GuantanamoPicha: AP

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Rais Barack Obama mara tu alipoingia madarakani January mwaka huu kutangaza kuwa jela hiyo itafungwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujayo.Lakini hata hivyo anakabiliwa na ugumu wa wapi pa kuwapeleka mahabusu waliyoko katika jela hiyo.


Kwa muda wa siku mbili kamishna wa sheria wa Umoja wa Ulaya Jacques Barrot pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamuhuri ya Czech ambayo ndiyo inayoshikilia kiti cha urais wa Umoja wa Ulaya,Ivan Langer wamekuwa mjini Washington kwa mazungumzo na maafisa wa Marekani.


Katika siku ya kwanza hapo jana ujumbe huo wa Umoja wa Ulaya ulikutana na Waziri wa Sheria wa Marekani Eric Holder na kumpatia orodha ya maswali ambayo umoja huo unahitaji kupata majibu kutoka Marekani kuhusiana na suala hilo la mahabusu wa gereza la Guantanamo.


Ikumbukwe ya kwamba serikali ya Marekani imewasilisha ombi kwa nchi za Umoja wa Ulaya kuwapokea baadhi ya mahabusu waliyoko katika gereza hilo.

Waziri wa Sheria wa Jamuhuri ya Czech Ivan Langer hata hivyo amesema kuwa ujumbe huo wa umoja wa ulaya hauna mamlaka ya kufikia makubaliano yoyote na Washington zaidi ya kuwasilisha maswali na kupokea majibu au taarifa.


´´Sisi hatuna mamlaka yoyote kutoka baraza la mawaziri wa mambo ya ndani ya kujadiliana, lakini ni kupokea na kutoa taarifa, Na tumeona kuwa serikali ya Marekani iko makini na suala hili.Tumeeleza kuwa kuna nchi ambazo ziko tayari kuwapokea mahabusu wa gereza la Guantanamo, pia kuna nchi ambazo ziko tayari kuwapokea lakini chini ya usimamizi wa Umoja wa Ulaya.Na kuna nchi nyingine haziko tayari kuwapokea mahabusu hao, na ndiyo maana jukumu langu hapa ni kuwasilisha kitu kama mtizamo wa pamoja´´


Kwa mujibu wa wajumbe hao wa Umoja wa Ulaya, maswali hayo ni pamoja na majaaliwa ya mahabusu hao wa gereza la Guantanamo.


Kwa upande wake kamishna wa Umoja huo wa Ulaya, Jacques Barrot amesema kuwa pia umoja huo unataka kufahamu mengi zaidi kuhusiana na gereza la Marekani la Bagram huko Afghanistan, na kwamba umoja huo umewasilisha mapendekezo ya pamoja kuhusiana na gereza hilo.


´´Kile ambacho Wizara ya Nje imependekeza kwetu si mkataba ni makubaliano ambayo kimsingi tunaunda ushirikiano wa kupambana na ugaidi.Naamini kuwa Marekani inataka kufungua ukurasa mpya katika kushughulikia kwa dhati suala la mahabusu´´


Barrot amesema anahisi wamarekani wanataka kesi zote za mahubusu wa Guantanamo zichunguzwe, na kwamba hawajatupilia mbali nafasi ya nchi hiyo kuwachukua mahabusu hao.


Amesema kuwa Uhispania, Ureno Italia na Ufaransa ni miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya ambazo kimsingi zimekubali kuwachukua mahabusu hao


Lakini Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamuhuri ya Czech Ivan Langer amesema kuwa tarehe ya kuanza kutolewa mahabusu hao itapangwa pengine January mwakani wakati gereza hilo litakapofungwa na kwamba yote hayo yako kwa serikali ya Marekani.


´´Kasi ya kufanyika hayo sasa iko katika mikono ya wamarekani na hatua iliyopigwa katika majaaliwa ya mahabusu hao ni kwamba tumewapa orodha ya maswali kwa hiyo tunasubiri majibu, tunasubiri taarifa zaidi kuona jinsi ambavyo yanavyotakiwa kuwa, makubaliano yasiyokuwa rasmi.´´


Wakati wa ziara ya ujumbe huo wa Umoja wa Ulaya, pia suala la kuondolewa kwa vibali vya kuingia kati ya Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya lilijadiliwa.


Mpaka sasa kuna nchi tano za Umoja wa Ulaya ambazo wakaazi wake wanawajibika kuomba vibali vya kuingia Marekani yaani viza.