1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Ulaya zawaunga mkono Waukraine

Moh2 Februari 2014

Marekani na Umoja wa Ulaya wamebadilishana vijembe vikali visio vya kawaida na Urusi Jumamosi(01.02.2014) kuhusu mustakbali wa Ukraine huku kukiwa na wasi wasi wa jeshi kuingilia kati kuzima maandamano dhidi ya serikali.

https://p.dw.com/p/1B1JN
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akizungumza katika Mkutano wa Usalama mjini Munich,Ujerumani. (01.02.2014)
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akizungumza katika Mkutano wa Usalama mjini Munich,Ujerumani. (01.02.2014)Picha: Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema kile kinachotokea Ukraine ni muhimu kwa mustakbali wa Ulaya wakati mwenzake wa Urusi Segei Lavrov alijibu kauli hiyo kwa kushutumu uingiliaji kati wa makusudi na undumila kuwili wa mataifa ya magharibi.

Katika mkutano wa usalama mjini Munich Ujerumani ambapo wanadiplomasia wa mataifa ya magharibi wamepata fursa ya kukutana na viongozi wa upinzani wa Ukraine,Kerry amesema waandamanaji wanaoipinga serikali wanaamini kwamba mustakbali wao haulazimiki kutegemea nchi moja tu na hawapaswi kushurutishwa.

"Hakuna mahala leo ambapo mapambano ya demokrasia na mustakbali wa Ulaya ni muhimu kuliko Ukraine" amesema Kerry." Marekani na Umoja wa Ulaya wanawaunga mkono wananchi wa Ukraine katika mapambano hayo."

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akihutubia katika Mkutano wa Usalama mjini Munich,Ujerumani. (01.02.2014)
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akihutubia katika Mkutano wa Usalama mjini Munich,Ujerumani. (01.02.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Undumila kuwili

Kupangwa kwa mkutano wa Kerry na upinzani wa Ukraine yumkini kukafafanuwa kauli kali iliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ambaye ameyashutumu mataifa ya magharibi kwa kuchochea ghasia mjini Kiev ikiwa ni katika mfano wa wazi wa undumila kuwili wa mataifa hayo.

Lavrov ameuambia mkutano huo kwa nini wanasiasa wengi wa mataifa ya magharibi wanachochea hatua hizo wakati huko kwao wanakuwa haraka kuchukuwa hatua kali dhidi ya uvunjaji wa sheria.Amesema anashangazwa na uchocheaji zaidi wa ghasia za mitaani unahusiana vipi na suala la kuendeleza demokrasia.

Lavrov amesema kwa nini hawasikii kulaaniwa kwa wale wenye kushikilia majengo ya serikali, kuwashambulia na kuwatesa polisi na kutumia kauli mbiu za kibaguzi dhidi ya Uyahudi na Manazi?

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov katika Mkutano wa Usalama wa Munich. (31.01.2014).
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov katika Mkutano wa Usalama wa Munich. (31.01.2014).Picha: Reuters

Mapema Jumamosi chama cha kiongozi wa upinzani Arseniy Yatsenyuk kimesema amewatahadharisha maafisa wa Umoja wa Ulaya kwamba ni jambo linaloyumkinika kabisa kwa serikali ya Ukraine kutumia nguvu kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kulihusisha jeshi la Ukraine.

Wizara ya Ulinzi ya Ukraine ambapo huko nyuma ilisema haitoingilia kati kwenye mzozo huo pia imeonya kwamba kitendo cha waandamanaji kunyakuwa majengo ya serikali hakikubaliki na kwamba " kupamba moto kwa makabiliano hayo kunatishia haki ya nchi hiyo kujitawala."

Mustakbali wa Ukraine

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy ameliambia mojawapo ya jopo la mkutano huo kwamba Umoja wa Ulaya unataka kuwa na uhusiano mzuri na Urusi na hicho ni kipengele muhimu katika suala la amani na ustawi kwa Umoja wa Ulaya lakini wananchi wa Ukraine wana haki ya kuamuwa mustakbali wao wenyewe ambao ni mustkabali na Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier akizungumza juu ya msimamo mpya wa Ujerumani katika sera zake za kimataifa amesema Ujerumani inataka na itatowa kichocheo katika sera ya pamoja ya Umoja wa Ulaya ya mambo ya kigeni na usalama.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika Mkutano wa Usalama wa Munich. (01.02.2014).
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika Mkutano wa Usalama wa Munich. (01.02.2014).Picha: Reuters

Akigusia suala la uhusiano na Urusi Waziri Steinmeier ameshauri kuwapo kwa ushirikiano wa ndani na Urusi ili kuitatua migogoro.Juu ya mgogoro wa Ukraine,Steinmeier ametoa mwito kwa viongozi wa nchi hiyo wa kuyatekeleza, haraka na kwa ukamilifu yale waliyokubaliana na wapinzani .

Steinmeier pia amewataka wote wanaoshiriki kwenye mkutano wa mjini Munich wafanye juhudi ili kuleta suluhisho la amani nchini Ukraine.

Mataifa ya magharibi na Urusi yatafautiana

Mataifa ya magharibi na Urusi yamekuwa yakitafautiana juu ya Ukraine tokea Rais Viktor Yanukovych alipoyatelekeza makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya hapo mwezi wa Novemba kutokana na shinikizo kutoka Urusi ambayo imekuwa ikijaribu kurudisha kwenye kundi lenye ushawishi wake jimbo lake hilo la zamani

Uamuzi huo wa Yanukovych umezusha maandamano makubwa ya kupinga serikali ambayo mwezi uliopita yaligeuka kuwa ghasia za matumizi ya nguvu baada ya rais kuchukuwa hatua kadhaa za kutaka kuyadhibiti maandamano hayo. Hatua zake hizo zilizidi kuchochea maandamano hayo mitaani ambapo rais baadae alilazimika kuzifuta na kukubali kujiuzulu kwa serikali.

Polisi wa kuzuiya fujo mjini Kiev,Ukraine.(31.01.2014)
Polisi wa kuzuiya fujo mjini Kiev,Ukraine.(31.01.2014)Picha: Reuters

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton anatarajiwa kizuru tena Kiev wiki ijayo baada ya hapo awali kukutana kwa mara kadhaa na viongozi wa upinzani na serikali mjini humo kutafuta ufumbuzi wa amani kwa mzozo huo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri:Mtullya Abdu.