1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuongeza wanajeshi Afghanistan

Lilian Mtono
19 Septemba 2017

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Jim Mattis amesema wataongeza wanajeshi 3,000 Afghanistan, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mpya wa Rais Donald Trump wa kuimarisha usalama katika nchi hiyo iliyoathirika na vita.

https://p.dw.com/p/2kImj
UN Generalversammlung in New York | Donald Trump, Präsident USA
Picha: Reuters/S. Stapleton

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Jim Mattis amesema nchi hiyo itaongeza wanajeshi 3,000 zaidi nchini Afghanistan, hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mpya wa Rais Donald Trump katika kuimarisha hali ya usalama katika nchi hiyo iliyoathirika kwa kiasi kikubwa na vita. 

Mwezi uliopita, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza sera mpya ya kuwafurusha wapiganaji wa Taliban, ambao wanaendeleza mashambulizi ya kutisha, na kuzingira maeneo makubwa nchini humo, huku wakuwaua maelfu ya wanajeshi wa vikosi vya Afghanistan. 

Mattis hapo jana aliiwaambia waandishi wa habari wa wizara ya ulinzi kwamba hakutaka kutoa idadi kamili ya wanajeshi watakaotumwa, ingawa alisema watatuma wanajeshi 3,000 nchini Afghanistan, ambao wataongeza nguvu kwa wanajeshi wengine takriban 11,000 wa Marekani ambapo tayari wapo nchini humo.

Afghanistan - US Soldaten am Ort eines Selbstmordanschlags der Taliban
Wanajeshi wa Mareakni wanakabiliana na wapiganaji wa Taliban nchini AfghanistanPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/S. Seiam

Majenerali wa Marekani kwa miezi kadhaa wamekuwa wakielezea hali ilivyo nchini Afghanistan kwa kuiita kuwa ni "mkwamo", licha ya misaada ya miaka kadhaa kwa washirika wa Afghanistan, msaada unaoendelea kutolewa na na jumuiya ya kujihami ya NATO na gharama ya jumla katika vita na ujenzi upya kwa Marekani kufikia zaidi ya Dola Trilioni 1.

Trump ambaye hapo awali alitetea kuhusu kuondolewa kwa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan, alibadilisha mawazo yake baada ya viongozi wa kijeshi wa Marekani kumshawishi kwamba gharama za kuyaondoa majeshi zitakuwa kubwa zaidi ya majeshi hayo kusalia.

Mkakati huo mpya wa Rais Trump kuhusu Afghanistan utafungua ukurasa mpya wa jitihada zilizofanikiwa za miaka miwili iliyopita za Marekani kuimarisha vikosi vya Iraqi dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS kwa mafunzo bora zaidi, msaada wa vifaa na kuunga mkono mashambulizi ya kijeshi kwenye maeneo yaliyozingirwa na maadui.

Afghanistan Selbstmordattentat in Kabul
Askari wa Afghanistan katika moja ya jumba lililolipuliwa na bomuPicha: Reuters/O. Sobhani

Marekani pia inazishinikiza nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO kuongeza idadi ya wanajeshi wao nchini Afghanistan. Marekani ilituma majeshi yake Afghanistan baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mnamo mwaka 2001, na hivyo kuufanya mzozo wa Afghanistan kuwa mrefu zaidi ambao Marekani imejihusisha nao. Hivi sasa Marekani ina wanajeshi 11,000 nchini humo.

Kundi la wanamgambo la Taliban linadhibiti asilimia 11 ya Afghanistan huku asilimia nyingine 30 ya eneo la nchi hiyo inazozaniwa kati ya serikali na wanamgambo. Kundi la wanamgambo wenye itikadi kali la Dola la Kiislamu IS pia limekita kambi nchini humo.

Aidha, Baraza la Seneti nchini Marekani limeidhinisha mswada wa ulinzi ambao utapiga jeki bajeti ya jeshi kwa kima cha dola bilioni 700, hiyo ikiwa bajeti kubwa zaidi kwa jeshi hilo katika kipindi cha miongo kadha ili kupambana katika vita vya Afghanistan na Iraq.

Seneti lilipitisha mswada huo kwa kura 89 dhidi ya 8 hapo jana kuidhinisha kuongezwa kwa bajeti ya jeshi kuanzia tarehe 1 mwezi ujao ili kuongeza uwezo wa Jeshi katika kukabilina na kuongezeka kwa kitisho kutoka Korea Kaskazini na kukataa kambi zaidi za kijeshi kufungwa.

Mswada huo wa kuongeza bajeti ya Jeshi la Marekani umemsaidia Rais Trump kutimiza mojawapo ya ahadi zake wakati wa kampeini za kulipa nguvu zaidi Jeshi hilo ambalo alisema lilipwaya wakati wa utawala wa mtangulizi wake Barack Obama.

Mwandishi: Lilian Mtono/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman