1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia

Admin.WagnerD17 Mei 2014

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amewaahidi viongozi wa Israel kwamba Marekani itafanya kile inacholazimika kufanya kuzuia Iran kuwa taifa lenye kumiliki silaha za nyuklia

https://p.dw.com/p/1C1VN
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel.Picha: Reuters

Waziri huyo wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel ametowa tamko hilo hadharani Ijumaa (16.05.2014) katika taarifa wakati wa mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem.Hagel amekaririwa akisema " nataka kuwahakikishia juu ya kujitolea kwa Marekani kuona kwamba Iran haimiliki silaha za nyuklia na kwamba Marekani itafanya kile wanachopaswa kufanya kutimiza ahadi hiyo."

Wote wawili wamezungumzia juu ya mpango tata wa nyukilia wa Iran ambao ulikuwa mada ya mazungumzo wiki hii mjini Vienna Austria kati ya mataifa makubwa ya magharibi na Iran. Netanyahu amesema katika taarifa akiwa amesimama pembezoni mwa Hagel kwamba wamekuwa wakisema kwa muda mrefu kuwa Iran inajaribu kuifumba macho jumuiya ya kimataifa kwa kuibabaisha.

Ameitaja repoti ya Umoja wa Mataifa kwa kile alichokiita juhudi zinazoendelea za Iran kuidanganya jumuiya ya kimataifa kuendelea kurutubisha kwa kiwango kikubwa madini ya urani kufikia uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia na kuendelea kukiuka ahadi zake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye kuipiga marufuku kuendeleza sehemu fulani za mpango wake huo wa nyuklia.

Maayatollah wadhibitiwe

Netanyahu amesema wanaendelea kufanya hivyo na anafikiri jambo hilo linahitaji kuwa na sera madhubuti kwa upande wa mataifa makubwa duniani. Kiongozi huyo wa Israel amesema lazima wasikubali kuwaachia maayatollah washinde kwa hilo, lazima wasiliwachie taifa hilo kubwa kabisa la kigaidi la Iran katika enzi hii kujijengea uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: picture-alliance/dpa

Akiwa nchini Israel,Hagel hapo Alhamisi alifanya ziara fupi katika kambi moja ya anga ambapo vikosi vya Marekani na Israel vinajiandaa kuanza mazoezi ya pamoja ya makombora ya kujihami yaliopewa jina la "Junior Cobra" kwa kutumia uigizaji wa kompyuta mithili kunapotokea hali ya mashambulio na namna ya kukabiliana na maafa baada ya kutokea mashambulizi.

Waziri wa mambo ya ulinzi wa Marekani alikuwa akikamilisha ziara yake ya siku nne Mashariki ya Kati ambayo ilianza Jumanne wiki hii mjini Jeddah Saudi Arabia ambapo alikutana na mawaziri wa ulinzi kutoka mataifa ya Ghuba ya Uajemi yenye uhusiano wa muda mrefu wa masuala ya usalama na Marekani.

Washirika hawatotelekezwa

Ziara ya Hagel inafanyika sambamba na mazungumzo ya kimataifa na Iran mjini Vienna yenye lengo la kurasimu makubaliano ya kuuwekea vikomo mpango huo wa nyuklia wa Iran ambalo ni suala linalopewa kipau mbele na mataifa ya Kiarabu yalioko Ghuba halikadhalika na Israel.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel (Kulia) na Mwana Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz al-Saud mjini Jeddah.(14.05.2014)
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel (Kulia) na Mwana Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz al-Saud mjini Jeddah.(14.05.2014)Picha: Getty Images

Serikali ya Iran inasema haina nia ya kutengeneza bomu la nyuklia.

Suala la kuboresha uhusiano na Iran limekuwa kipau mbele katika sera ya kigeni ya Rais Barack Obama wa Marekani na mazungumzo ya Vienna yameleta matumaini ya maana katika suala hilo la nyuklia. Akiwa nchini Saudi Arabia Hagel amesema kwamba katika mazingira yoyote yale Marekani haitoyatolea muhanga maslahi ya washirika wake ili kwamba ifikie makubaliano ya nyuklia na Iran.

Kwa kiasi kikubwa mazungumzo ya Hagel nchini Saudi Arabia yalikuwa yamekusudiwa kuzishawishi nchi za Ghuba ambapo mara nyengine zinakuwa na mvutano kushirikiana katika masuala ya kuwa na makombora ya kujihami pamoja na masuala mengine ya usalama.Nchi hizo zimekubaliana kukutana mara kwa mara kujadili masuala hayo lakini hazikutangaza hatua mpya katika kuwa na mfumo wa pamoja wa ulinzi wa anga na makombora ya kujihami.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/AFP
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman