1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuipatia Misri helikopta za mashambulizi

Admin.WagnerD23 Aprili 2014

Marekani imetangaza kuwa itaipatia Misri helikopta 10 za kijeshi aina ya Apache, katika hatua inayoashiria kulegezwa kwa hatua ya kusitisha msaada kwa taifa hilo, kufuatia mapinduzi ya mwaka jana.

https://p.dw.com/p/1BmX5
Apache Kampfhelikopter
Picha: Jeff J Mitchell/Getty Images

Maafisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon, walisema licha ya wasiwasi kuhusu kushindwa kwa Misri kutekeleza mageuzi ya kidemokrasia baada ya kumuangusha rais Mursi, serikali ya Marekan itaipatia Misri Helikopta 10 za kijeshi aina ya Apache. Pentagon ilisema katika taarifa kuwa waziri Chuck Hagel alimuarifu mwenzake wa Misri Jenerali Sedki Sobhy juu ya uamuzi huo wa rais Barack Obama, katika mazungumzo kwa njia ya simu jana Jumanne.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel.Picha: Reuters

Kuimarisha operesheni za Sinai

Msemaji wa waziri Hagel, admeli John Kirby, alisema helikopta hizo zitasaidia kuimarisha operesheni za kupambana na ugaidi katika rasi ya Sinai. Waziri wa mambo ya nchi za nje John Kerry alisafisha njia ya kuwasilisha ndege hizo kwa Misri, kwa kulihakikishia bunge la Marekani kuwa Misri imetimiza masharti muhimu kwa Marekani kurejesha sehemu ya msaada.

Masharti hayo yalihusisha Misri kuendelea kutekeleza majukumu yake chini ya mkataba wa amani kati yake na Israel. Lakini Kerry alibainisha katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri Nabil Fahmy, kuwa hajapata uthibitisho kuwa Misri ilikuwa inachukuwa hatua kurudi katika mkondo wa demokrasia.

Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema hakuna msaada zaidi wa kijeshi mbali na helikopta hizo za Apache zilizotengenezwa na kampuni ya Boeing, unatolewa kwa Misri kwa sasa. Hii inamaanisha kuwa utolewaji wa zana nyingine za kijeshi, kama vile ndege za kivita aina ya F-16 unaendelea kusimamishwa.

Mkuu wa zamani wa jeshi la Misri Abdel-Fatah Al-Sissi aliengoza mapinduzi dhidi ya rais Mursi.
Mkuu wa zamani wa jeshi la Misri Abdel-Fatah Al-Sissi aliengoza mapinduzi dhidi ya rais Mursi.Picha: Jacquelyn Martin/AFP/Getty Images

Ukiukaji w ahaki za binaadamu waendelea

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Jennipher Psaki, alisema waziri Kerry aliitaka Misri katika mazungumzo na mwenzake Fahmy, kuheshimu ahadi yake ya kurejea katika mkondo wa demokrasia, ikiwemo kuendesha uchaguzi huru, wa wazi na wa haki. Kerry pia aliitaka Misri kuelegeza udhibiti wa uhuru wa kujieleza, kufanya mikutano na wa vyombo vya habari.

Lakini hatua hii ya Marekani inaweza kuchochea wasiwasi miongoni mwa watetezi wa haki za binaadamu. Shirika la Human Rights Watch liliitahadharisha Washington mapema mwezi huu, dhidi ya kurejesha msaada wa kijeshi kwa Misri, hadi serikali ya nchi hiyo itakapokomeshe vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu, na kuwawajibisha wanaoendesha vitendo hivyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Saum Yusuf