1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Iran washirika wa lazima Irak

13 Agosti 2014

Irak imepata waziri mkuu mpya na kuonekana ikiondoka kwenye mkwamo wa kisiasa, lakini Jamsheed Faroughi wa Idhaa ya Kifarsi ya DW anasema nchi hiyo inakabiliana na mkwamo zaidi ya mmoja.

https://p.dw.com/p/1CtIB
Wakimbizi wa jamii ya Yazidi katika Mlima Sinjar.
Wakimbizi wa jamii ya Yazidi katika Mlima Sinjar.Picha: Reuters

Kwa sasa Irak inapaswa kushindana na migogoro miwili inayotishia maisha yake kama taifa: mgogoro wa kisiasa kutokana na kugombea madaraka baina ya makundi yenye ushawishi, na pia mgogoro wa kile kinachoitwa "Dola ya Kiislamu" inayoibuka pachikoni mwa kundi la kigaidi kaskazini mwa nchi hiyo. Migogoro yote miwili, hata hivyo, inahusiana. Kwenye uundikaji wake, zote, Marekani na Iran, zina sehemu zao.

Wamerekani wanahusika kwa kiasi fulani kwani uvamizi wao nchini Irak na sera zao zimehujumu takribani taasisi zote za kisiasa. Matokeo yake hali ya usalama imezorota kwa kasi ya kutisha. Vita vya Irak vilikuwa kosa kubwa sana, hilo hakuna ambaye anaweza kulitilia shaka. Lakini hisia za mkosaji na kujirudi hakutoi suluhisho lolote lenye manufaa.

Jamsheed Faroughi wa Idhaa ya Kifursi ya DW.
Jamsheed Faroughi wa Idhaa ya Kifursi ya DW.Picha: DW/P. Henriksen

Mkono wa Iran

Ma-ayatullah wa Iran nao wanahusika kwa kiasi na wanabeba dhamana kwa sababu waliitumia fursa ya ukosefu wa nguvu yenye ushawishi iliyoachwa na dikteta Saddam Hussein kwa maslahi yao, huku Waziri Mkuu Nouri al-Maliki akiwa mtu mwenye mafungamano mazuri sana na Iran.

Katika kipindi chake cha uongozi, Maliki amefanya kile hasa ambacho ma-Ayatullah wa Iran wamekuwa wakikifanya tangu kale, nacho ni kuzikabidhisha nguvu zote za kisiasa kwenye mikono ya Shia na kuzuia ushiriki wowote wa kisiasa kutoka kwa Sunni.

Hayo nayo yalikuwa ni makosa makubwa yenye matokeo makubwa pia. Kutokuridhika kwa Sunni kuliwasukuma vijana wengi kwenye mikono ya makundi ya siasa kali. Ukosefu wa taasisi za kiusalama na upuuziaji wa Marekani vikafanya kazi iliyobakia, ambayo matokeo yake ni kusonga mbele kwa kasi ya ajabu kwa wanamgambo wa kundi la “Dola ya Kiislamu“ nchini Irak.

Muungano wa lazima

Yote yalianza mwaka 2003 kama muungano wa wenye dhamira, sasa unaweza kuuita kirahisi zaidi kuwa ni muungano wa wasio dhamira. Sasa ushirikiano wa Marekani na Iran, hapana shaka, si ushirikiano wa hiari, lakini hakuna si Washington wala Tehran peke yake yenye uwezo peke yake kuzuia ukatili wa hilo kundi lijiitalo Dola ya Kiislamu.

Marekani ina nguvu za kijeshi zinazohitajika, Iran ina nguvu za kisiasa zinazohitajika. Kwa maneno mengine, kila mmoja anapaswa kuutatua mzozo huu kwa kiwango kikubwa kadiri anavyohusika. Marekani haina njia ila kuituliza hali mbaya ya kiusalama kaskazini mwa Irak. Iran nayo lazima itumie ushawishi wake nchini Irak kuleta amani kwenye eneo hilo. Na hilo litawezekana tu kwa maridhiano na Sunni.

Bila ya jitihada za pamoja za Iran na Marekani, kuporomoka kwa Irak ni jambo linalowezekana sasa. Hilo litakuwa hatari pia kwa wale wanaopakana na nchi hiyo, kwani linaweza kuzitia nchi kama Iran kwenye miongo kadhaa ya machafuko. Jumuiya ya kimataifa itailaumu Marekani na hivyo, hakuna njia mbadala zaidi ya ushirikiano wa maadui hawa wakubwa.

Mwandishi: Jamsheed Faroughi
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba