Marais wa Israel na Palastina wahutubia bunge la Uturuki | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.11.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marais wa Israel na Palastina wahutubia bunge la Uturuki

Ulikuwa wakati wa kihistoria. Kwa kuwahutubia jana wabunge wa Kituruki huko mjini Ankara, Shimon Perez alikuwa rais wa kwanza wa Israel kulihutubia bunge la nchi ya Kiislamu. Hapo kabla Shimon Perez alikutana na mwenzake wa Palastina, Mahmoud Abbas, ambaye pia alilihutubia bunge hilo.

Rais Abdullah Gül wa Uturuki (kulia ) na Rais Shimon Perez wa Israel

Rais Abdullah Gül wa Uturuki (kulia ) na Rais Shimon Perez wa Israel

La muhimu vichwani mwa watu hao wawili ni mustakbali wa mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati, lakini zaidi pia ni namna Uturuki itakavojishughulisha kikweli katika maeneo ya Wapalastina kwa kushirikiana na Wa-Israeli.

Kwa miaka mingi Israel na Uturuki zimekuwa na uhusiano wa karibu na wa kirafiki. Nchi mbili hizo zinashirikiana katika nyanja nyingi, ikiwa pia katika masuala ya kijeshi. Lakini lazima ichukuliwe kuwa ni tokeo maalum pale rais wa Israel anapoingia na kulihutubia bunge la Uturuki, tena kwa lugha ya Ki-Hibrew. Shimon Perez amefanya ziara za kila wakati huko Misri na Jordan, lakini huko hajawahi kupewa heshima ya aina hiyo.

Kwamba sasa ameweza kuingia na kulihutubia bunge la Ankara ni jambo linalofaa kutiliwa maanani sana. Shimon Perez hajaingia katika bunge hilo akiwa peke yake, lakini pia Rais Mahmoud Abbas wa Palastina alitoa hotuba. Sababu ya mwanzo ni kwamba Uturuki pamoja na Israel na Wapalastina wanataka waunde eneo la pamoja la kiviwanda katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Wakati huo huo,lakini, mwaliko huu wa Uturuki kwa Shimon Peres na Mahmoud Abbas unadhihirisha namna nchi hiyo ilivokusudia kikweli kutoa mchango madhubuti katika juhudi za kuweko utaratibu wa amani katika Mashariki ya Kati.

Lakini itakuwa kutia chumvi pale mtu anapoposema kwamba Uturuki itakuwa mpatanishi katika juhudi hizo. Uturuki inaweza ikasaidia kwa kuchukua hatua za kivitendo, na kusonga mbele kwa kutoa mifano mizuri, ambapo wengine wanaweza na wanahitajika kuchangia. Itakuwa kuivisha Uturuki viyatu vikubwa sana zaidi kuliko ukubwa wa miguu yake pale mtu atakapotarji kwamba nchi hiyo itakuwa mpatanishi barabara. Viatu hivyo tangu hapo ni vikubwa hata kwa nchi za Ulaya.

Anayeweza kukivaa viatu vya upatanishi hivi sasa ni tu Marekani, ambayo bado inazubaa katika jambo hilo. Hadi sasa hiajaweza kutangaza wazi wazi kama mkutano wa Mashariki ya Kati uliopangwa kufanywa Annapolis mwisho wa mwezi huu wa Novemba kweli sasa utafanyika. Pia Marekani haijaweka wazi vipi mkutano huo utajiwajbisha kuelekea mwenendo wa amani.

Hamna mtu anayejuwa zaidi juu ya mambo hayo kuliko Wa-Israeli na Wapalastina. Shimon Perez na Mahmoud Abbas walizungumza wakitiwa moyo juu ya nafasi ya kupatijkana amani, lakini katika matamshi yao mtu aliweza kugundua wazi kwamba tafauti baina ya misimamo ya pande hizo mbili bado ingaliko, kuna tafauti kubwa. Kila upande unautegemea upande mwengine uregeze kamba. Kwa mfano Wa-Israeli wanatakiwa lazima wayaondoshe makaazi yao ya kilowezi katika ardhi ya Wapalastina, huku Israel ikiwataka Wa-Israeli waitambuwe dola hiyo ya Kiyahudi kabla hata kuanza kuzungumzia juu ya amani. Ni uzuri kwamba Shimon Perez na Mahmoud Abbas wamekuweko Uturuki. Lakini kuhusu amani mambo hayajabadilika, kuna bado pengo baina yao.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com