1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano zaidi Syria

MjahidA14 Januari 2013

Mashambulizi ya angani katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi kusini magharibi mwa mji wa Damascus nchini Syria, yamesababisha vifo vya takriban watu ishirini

https://p.dw.com/p/17JQ0
Jengo lililoharibika kwa mashambulizi
Jengo lililoharibika kwa mashambuliziPicha: Reuters

Kulingana na mwanaharakati anayeishi katika eneo la Moadamiyeh, ambaye hakutaka jina lake litajwe, waliouwawa ni kutoka familia mbili tofauti na wengi ni wanawake na watoto. Picha za video za wanaharakati hao zimeonyesha mwili wa mtoto mdogo wa kiume ukivutwa kutoka vifusi vya jengo lililoshambuliwa ukiwa umejaa vumbi na damu.

Kwa upande wake shirika la kutetea haki za binaadamu lililo na makao yake mjini London limesema lina majina ya watoto saba waliouwawa katika shambulizi hilo. Shirika hilo limesema kuna uwezekano wa idadi ya vifo kupanda kwa kuwa waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.

Baadhi ya vikosi vya serikali
Baadhi ya vikosi vya serikaliPicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo ni vigumu kujua hali halisi ya mambo yanavyoendelea nchini Syria kwa sababu serikali ya Bashar Al Assad imepiga marufuku vyombo vya habari vya kujitegemea. Hapo jana vikosi vya serikali pia vilifanya mashambulizi katika eneo la mashariki mwa mji wa Damascus na kuuwa watu 36 wakiwemo watoto 14.

Tangu kuanza kwa mapigano nchini humo miezi 21 iliopita takriban watu 60,000 wameuwawa huku wengine wengi wakiachwa bila makao na wengine kukimbilia nchi jirani.

Mahema yanayokaliwa na wakimbizi wa Syria
Mahema yanayokaliwa na wakimbizi wa SyriaPicha: Karen Leigh

Kwengineko waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema upinzani nchini Syria unapaswa kufuata matakwa ya Assad katika hotuba yake ya hapo awali kwamba waanzishe mazungumzo na serikali ya Assad ili kumaliza umwagikaji wa damu nchini humo.

Urusi yahimiza mazungumzo ya amani

Lavrov amesema iwapo angekuwa upande wa upinzani angetafuta kila njia ya kufanikisha mazungumzo na serikali.

Urusi ambayo mara nyingi imekuwa ikitumia kura yake ya turufu kupinga hatua kuchukuliwa dhidi ya mshirika wake jambo ambalo limeiweka urusi katika mahusiano mabaya na mataifa ya magharibi na hata yale ya kiarabu inasema kwamba mapendekezo ya Assad yana uzito na yanapaswa kuzingatiwa.

Waziri wa nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa nchi za nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: picture-alliance/dpa

Hii leo kamati ya kimataifa ya uokozi ya Marekani IRC, imeihimiza dunia nzima kutia juhudi zaidi katika kufadhili mipango ya kusaidia kupata msaada wa kutosha wa kibinaadamu nchini Syria. Zaidi ya watu 600,000 wamekimbia mapigano ya nchini Syria na kwenda nchini Uturuki, Lebanon, Jordan, na Iraq.

Kuna zaidi ya watu milioni 2 waliopoteza makaazi yao nchini Syria na Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa kwa sasa ni watu milioni 4 wanaohita msaada wa kibinaadamu.

Mwandishi Amina Abubakar/Reuters/AP/dpa

Mhariri Yusuf Saumu