1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazuka tena Somalia,watano wauwawa.

Sekione Kitojo18 Aprili 2007

Mapigano mapya baina ya majeshi ya Ethiopia na wapiganaji wa Kisomali yamesababisha watu takriban watano kuuwawa mjini Mogadishu , kwa mujibu wa wakaazi wa mji huo.

https://p.dw.com/p/CB4e
Wasomali wakimbia Mogadishu
Wasomali wakimbia MogadishuPicha: AP

Mapigano makali ya makombora yamelitikisa eneo la kusini mwa mji mkuu Mogadishu usiku wa Jumanne, na baadhi ya makombora yameangukia karibu na jumba la rais.

Nimeona miili ya watu watatu ikiondolewa kutoka katika nyumba iliyopigwa makombora, Abdirahman Bile, mkaazi ya kitongoji cha Towfiq ameliambia shirika la habari la Reuters.

Mwandishi mmoja wa habari raia wa Kisomali amesema kuwa mtu mwingine ameuwawa katika soko la Bakarah na mwingine katika wilaya ya Karaan kaskazini ya mji wa Mogadishu.

Nae Ibrahim Helmi mwandishi wa habari wa radio Shebele ya mjini Mogadishu akizungumza na radio Deutsche Welle idhaa ya Kiswahili hivi punde amesema kuwa maeneo yote katika mji huo yako katika hatari.

Msemaji wa ukoo maarufu katika mji wa Mogadishu wa Hawiye amesema makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya wapiganaji na majeshi ya Ethiopia yanayosaidia serikali kuudhibiti mji huo uliokumbwa na mapigano bado yanaendelea.

Hadi pale majeshi hayo yatakapotenganishwa, matukio kama haya yataendelea kutokea, amesema Ahmed Diriye Diriye, msemaji wa ukoo wa Hawiye, akiongeza kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano hayajavunjika.

Wapiganaji hao wanatoka katika ukoo wa Hawiye na wanaharakati wa kundi la Kiislamu, ambao hapo kabla walijulikana kama baraza la mahakama za Kiislamu nchini Somalia.

Majeshi ya Ethiopia na yale ya Somalia yamelishinda jeshi la mahakama za Kiislamu , ambalo lilikuwa na uungwaji mkono wa ukoo wa Hawiye na kutawala sehemu ya kusini ya Somalia kwa muda wa nusu ya mwaka 2006, kutokana na vita iliyochukua muda mfupi katika wakati wa mwaka mpya.

Mkaazi mwingine wa Mogadishu ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mapigano ya jana Jumanne yalikuwa makali kuliko mapigano yaliyozuka kati ya tarehe 29 mwezi wa March na Aprili mosi ambapo watu 1,000 waliuwawa na zaidi ya watu laki mbili waliyakimbia makaazi yao.

Mapigano ya jana usiku yalikuwa makubwa kuliko mapigano yaliyodumu kwa muda wa siku nne, kitu ambacho hakikuwapo ni helikopta za kijeshi tu angani , lakini ukali wa mapigano hasa kurushwa kwa makombora kulikuwa ni sawa na mapigano ya wakati mwingine, amesema mkaazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Baadhi ya watu wamesema kuwa wamelala msikitini kwa kuwa hawakuweza kuvumilia kulala majumbani mwao. Kombora moja liliangukia katika paa la kiwanda cha kuoka mikate cha Baar Ubax ambacho hutengeneza mikate kwa ajili ya eneo kubwa la mji huo lakini wafanyakazi wamesema kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa.