1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazidi Ukanda wa Gaza

Mjahida25 Julai 2014

Ndege za kivita ya Israel zimezishambulia takribani nyumba 30 ndani ya Ukanda wa Gaza, na kusababisha mauaji kadhaa yakiwemo ya kiongozi mmoja wa Hamas na wanawe wawili wa kiume

https://p.dw.com/p/1CirA
Mashambulizi katika Ukanda wa Gaza
Mashambulizi katika Ukanda wa GazaPicha: Reuters

Msemaji wa polisi mjini Gaza, Ayman Batniji, amemtaja kiongozi huyo wa Hamas aliyeuawa asubuhi ya leo katika mji wa Rafah kuwa ni Salah Hassanein, wanawe wawili wa kiume walio na miaka 12 na 15 pamoja na mama mja mzito.

Vifo hivi vimeongeza idadi ya watu waliouwawa kufikia 808 tangu Israel ilipoanzisha hujuma yake dhidi ya Ukanda wa Gaza siku 18 zilizopita.

Kwa upande wa Israel, watu 34 ndio waliouwawa wakiwemo wanajeshi 32.

Baadhi ya familia zikiomboleza wapendwa wao waliouwawa
Baadhi ya familia zikiomboleza wapendwa wao waliouwawaPicha: Reuters

Huku hayo yakiarifiwa baraza la usalama nchini Israel linakutana baadaye leo kujadili iwapo wapanue oparesheni yao zaidi dhidi ya Hamas au wazingatie mwito wa kusimamisha mapigano.

Hana Amireh, afisa mkuu wa chama cha ukombozi la Palestina amesema miongoni mwa yaliyomo kwenye mkataba wa amani ni mwito wa siku tano za kusimamisha mapigano, ambapo Israel na Hamas wanatarajiwa kujadiliana juu ya mfumo mpya wa mpakani katika eneo lililofungiwa la Gaza.

Waziri Mkuu wa Uturuki aelekea Qatar kwa juhudi za amani

Lakini Hamas imesema haitosimamisha mapigano bila hakikisho kutoka kwa jamii ya kimataifa kwamba Misri na Israel itafungua mpaka wa Gaza baada ya kuufunga kwa takribani miaka saba. Bado Misri na Israel hazijaridhia sharti hilo kwa kuhofia huenda ikawapa nguvu zaidi wapiganaji wa Hamas.

Kwa upande mwengine, maelfu ya watu nchini Iran wameingia mitaano hivi leo kuadhimisha kile kinachoitwa "Siku ya Quds" ambayo hufanywa kila Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kuwaunga mkono Wapalestina.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu
Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet DavutogluPicha: picture-alliance/dpa

Maandamano yanafanyika mjini Tehran na katika miji mengine takriban 700 katika taifa hilo la Kiislamu. Waandamanaji walionekana wakibeba mapango yalioandikwa "Kifo kwa Marekani, Kifo kwa Israel".

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, ambaye nchi yake inashiriki juhudi za kusaka makubaliano ya kusitisha amani, amefuta ziara yake ya Ufaransa na badala yake ameelekea Qatar kwa mazungumzo na wawakilishi wa Israel na Hamas.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef