1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazidi kuinyemelea Damascus

13 Desemba 2012

Bomu lililotegwa kwenye gari limeuwa watu 16 nje ya mji mkuu wa Damascus leo masaa machache baada ya mripuko wa bomu kumjeruhi waziri wa mambo ya ndani wakati Urusi ikiungama kwamba utawala huo unaweza kushindwa na waasi

https://p.dw.com/p/1724y
Vita Vya Syria
Vita Vya SyriaPicha: Reuters

Miripuko hiyo ya mabomu imetokea nje ya eneo lenye nyumba za jeshi na karibu na shule ya msingi ambapo watoto saba ni miongoni mwa watu waliouwawa na wengine 23 wamejeruhiwa wengi wao wakiwa watoto.Miripuko hiyo ya leo inafuatia ile mitatu ya hapo jana dihidi ya wizara ya mambo ya ndani ambayo imeuwa takriban watu watano na kusababisha kulazwa hospitalini kwa Waziri wa mambo ya ndani Mohammed Ibrahim al- Shaar aliyejeruhiwa begani wakati dari la ofisi yake lilipoanguka.

Kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya maeneo ya serikali kunakuja baada ya serikali za nchi za Kiarabu na Mataifa ya Magharibi kuutambuwa upinzani wenye kuendesha harakati zake kwa kutumia silaha kuwa mwaklishi pekee halali wa wananchi wa Syria na wakati serikali ya Marekani ikisema kwamba jeshi linalozidi kuemewa likiamuwa kutumia makombora ya masafa marefu na mabomu ya kuteketeza dhidi ya waasi.

Muungano wa Kitaifa wahamasishwa

Hapo jana zaidi ya nchi 100 zimeutambuwa muungano mpya wa Syria na hiyo kufunguwa njia ya kupatiwa kwa msaada mkubwa zaidi kwa vikosi vinavyopigana kumpinduwa Rais Bashar al Assad ukiwemo uwezekano wa kupatiwa msaada wa kijeshi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akiwa na Sheikh Abdullah bin Zayed al Nahyan wakati wa mkutano wa 'Marafiki wa Syria ' uliofanyika Marrakesh,Morroco Jumatano (12.12.2012)
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akiwa na Sheikh Abdullah bin Zayed al Nahyan wakati wa mkutano wa 'Marafiki wa Syria ' uliofanyika Marrakesh,Morroco Jumatano (12.12.2012)Picha: picture-alliance/dpa

Shirika la habari la serikali nchini Syria SANA limewalaumu magaidi kwa miripuko ya leo hii katika eneo la makaazi la Qatana ambao ni mji unaodhibitiwa na jeshi kusini magharibi ya Damascus.Kwa mujibu wa shirika hilo asubuhi ya leo magaidi walishambulia makaazi ya raia ya Ras- al-Nabaa kwa kutumia gari lililosheheni mabomu na kuliripua mbele ya shule ya Mikhael Samaan.Mashambulizi hayo ambayo yanafanyika karibu kabisa na mji mkuu yanakuja kufuatia kutekwa na waasi kwa kambi muhimu katika wiki za hivi karibuni jambo ambalo limewapa udhibiti wa sehemu kubwa ya kaskazini magharibi na mashariki mwa nchi hiyo na kumfanya mwanadiplomasia mwandamizi wa Urusi kukiri kwamba kushindwa kwa mshirika huyo wa muda mrefu wa Urusi ni jambo linalowezekana.

Urusi haifuti uwezekano wa kuanguka utawala wa Syria

Naibu waziri wa mambo ya nje Mikhail Bogdanov amekaririwa na shirika la habari la ITAR-TASS akisema kwamba katika suala la waasi kujiandaa kwa ushindi bila ya shaka hilo ni jambo linalowezekana.Amesema kweli unaonekana machoni kwamba serikali inazidi kupoteza sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo.Kutekwa kwa kambi ya Sheikh Suleiman na waasi hapo Jumatatu kumewapa waasi udhibiti kamili wa ukanda wa ardhi unaoanzia kwenye viunga vya mji wa pili kwa ukubwa wa Allepo hadi kwenye mpaka na Uturuki.Kutambuliwa kwa Muungano wa Kitaifa wa upinzani wa Syria na Marekani pamoja na nchi nyenginezo kumezidi kuuhamasisha upinzani huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov, wa pili kulia akizungumza na waziri mwenzake wa Syria Walid Muallem wa pili kushoto Kulia ni naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Mikhail Bogdanov.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov, wa pili kulia akizungumza na waziri mwenzake wa Syria Walid Muallem wa pili kushoto Kulia ni naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Mikhail Bogdanov.Picha: AP

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu