1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yatulia Mashariki mwa Kongo

28 Oktoba 2013

Mapigano ya siku tatu mfululizo baina ya jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 katika miji ya Kiwanja, Rutshuru na Kibumba sasa yanaonekana kutulia, baada ya jeshi kuidhibiti miji hiyo.

https://p.dw.com/p/1A77g
Wanajeshi wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wanajeshi wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: picture-alliance/dpa

Mapigano hayo yaliyoanza Ijumaa iliyopita yaliendelea hadi jana Jumapili (tarehe 27 Oktoba) na kupelekea kuanguka kwa miji ya Kiwanja na Rutshuru katika mikono ya jeshi la serikali, likiungwa mkono na vikosi vya Umoja wa Mataigf nchini humo, MONUSCO.

Katika mapigano hayo, mwanajeshi mmoja wa Umoja wa Mataifa kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alipoteza maisha. Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Martin Kobler, amelaani vikali kuuawa kwa mwanajeshi huyo, ambaye amepoteza maisha yake wakati akitekeleza jukumu lake la kuwakinga raia wa kawaida.

Nao wakaazi wa mji wa Kiwanja, ambao kwa takribani mwaka moja sasa walikuwa chini ya uongozi wa M23, wamewakaribisha wanajeshi wa serikali kwa mayowe na nderemo, wakiomba kwamba wanajeshi hao wabaki kuwalinda daima.

Makaburi ya Halaiki

Gavana wa Mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Julien Paluku, aliutembelea mji mdogo wa Kibumba hivi karibuni na ametangaza kugunduliwa makaburi ya pamoja mawili katika mji mdogo wa Kibumba. Gavana huyo ameomba jumuia ya kimataifa pamoja na Monusco kuendesha uchunguzi wa kina ili waliohusika na uhalifu huo waadhibiwe.

Gari la Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Gari la Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Junior D. Kannah/AFP/Getty Images

"Ni uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu. Na ikiwa itabainika kuwa wahanga walifanyiwa unyama huo kutokana na kabila lao, ni mauwaji ya kimbari. Kwa hiyo nadhani kwamba MONUSCO pamoja na jumuia yote ya kimataifa, pamoja na mashirika ya kutetea haki za binaadamu, wanaalikwa kwa haraka kwenda huko iliwaliohusika wajulikane na hasa kwani eneo hilo lilikuwa chini ya uongozi wa M23 na kama ni M23 waliohusika wapelekwe mahakamani, na pia mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC ijulishwe."

Umoja wa Mataifa wawaalika M23 kujisalimisha

Na wakati vita vikiendelea, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo kimewafungulia milango wapiganaji wa M23 wajisalimishe. Hayo yalitangazwa na ofisa wa Tawi la Siasa katika MONUSCO Goma, Josuas Obate.

Mwanamke akipita mbele ya wanajeshi wa Kongo mkoani Kivu ya Kaskazini.
Mwanamke akipita mbele ya wanajeshi wa Kongo mkoani Kivu ya Kaskazini.Picha: Carl de Souza/AFP/Getty Images

Waasi wa M23,baada ya kupoteza miji ya Kiwanja na Rutshuru, kilomita 80 kaskazini ya mji wa Goma, wanaliomba jeshi la serikali kushimamisha vita ili kuendelea na mazungumzo ya mjini Kampala.

Msemaji wa chama hicho, Amani Kabasha, alisema ikiwa serikali haitashimamisha mapigano, watalazimika "kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya ngome za jeshi la serikali, FARDC."

Mwandishi: John Kanyunyu/DW Goma
Mhariri: Mohammed Khelef