1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yanaendelea Somalia

Oummilkheir22 Machi 2007

Risasi na mizinga inazidi kufyetuliwa Mogadischu na pia kaskazini ya Somalia

https://p.dw.com/p/CHHl
Wanajeshi wa Somalia wapiga doria Mogadischu
Wanajeshi wa Somalia wapiga doria MogadischuPicha: AP

Milio ya risasi za rashasha na mizinga imefyetuliwa hii leo katika mji mkuu wa Somalia Mogadischu ambako serikali inasema mapambano yataendelea hadi mpango wao wa kuwatimua waasi unakamilika.Wanamgambo wa kiislam kwa upande wao wanasema wataendelea kupigana hadi wanajeshi wa kigeni wanaihama nchi hiyo.

Mnamo siku ya pili ya mapigano makali kati ya waasi na wanajeshi wa serikali ya Somalia na wa Ethiopia,mapigano yaliyogharimu maisha ya watu wasiopungua 14,mamia ya wasomali wanayapa kisogo maskani yao kusini mwa mji mkuu Mogadischu.

Wanajeshi wa kisomali wamepiga doria usiku kucha katika mitaa kadhaa ya mji mkuu huo.

Maduka mengi yamefungwa hii leo,sawa na ilivyokua hapo jana.Magari ya kijeshi yanazunguka zunguka mitaani.

Tangu jana asubuhi,serikali ya mpito ya Somalia ikisaidiwa na wanajeshi wa Ethiopia,imeanzisha opereshini kubwa ya msako mitaani kuwapokonya silaha wanamgambo.

“Serikali inapambana na magaidi mjini Mogadischu.Mapigano hayatasita kabla hatujawavunja nguvu.Tutaendelea na juhudi zetu za kuleta hali ya utulivu mjini Mogadischu.Waasi hawataweza kutuzuwia kutekeleza mpango wetu”-amesema hii leo naibu waziri wa ulinzi wa Somalia Salad Ali Jelle wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari.

Bwana Jelle amewatuhumu waasi wa kiislam wanaoongozwa na Aden Hashi Ayro-kua nyuma ya hujuma dhidi ya kambi za jeshi la serikali mjini Mogadischu.

“Baada ya magaidi kushauriana na mtandao wa kigaidi wa Al Qaida,Ayro ameteuliwa kua mkuu wa Al Qaida mjini Mogadishu” ameongeza kusema naibu waziri wa ulinzi wa Somalia Salad Ali Jelle.Amewatolea mwito wakaazi wa Mogadischu waihame mitaa yote wanakojificha wanamgambo waliosalia wa kiislam.

Kwa upande wao wanamgambo hao wa kiislam wanasema wataendelea kupigana mpaka wanajeshi wote wa Ethiopia wanaihama Somalia.

Wanamgambo waliosalia wa kiislam wanailaumu jumuia ya kimataifa kwa kile wanachokiita “mapendeleo”.

Kiongozi wao Cheikh Hassan Dahir Aweys amehalalisha mashambulio ya papo kwa papo mjini Mogadischu,akisema “ni haki ya wasomali kujihami.”

Tangu wanamgambo wa kiislam walipotimuliwa nchini Somalia mwishoni mwa mwezi December uliopita,Mogadischu umegeuka kitovu cha mapambano ya umwagaji damu yanayoshuhudiwa takriban kila siku-yanayofanywa na makundi yanayobeba silaha ambayo serikali inawataja kua wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam.