1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yameenea katika maeneo mapya nchini Cote d'Ivoire

3 Machi 2011

Marekani imewaonya raia wake wasisafiri kwenda Cote d'Ivoire. Matangazo ya vyombo vya habari vya kimataifa yamefungwa Cote d'Ivoire huku rais Gbgabo akivilaumu kwa kuitingisha nchi

https://p.dw.com/p/10SiC
Gari ya polisi iliyochomwa moto katika kitongoji cha Abobo mjini AbidjanPicha: dapd

Milipuko imesikika katika kitongoji kimoja kusini mwa mji mkuu wa Cote d'Ivoire, Abidjan usiku kucha na hapo jana, huku mapigano kati ya waasi wanaotaka kumuondoa madarakani kiongozi anayeng'ang'ania madaraka nchini humo Laurent Gbagbo na vikosi vya usalama, kuenea katika maeneo mapya mjini humo. Wakaazi wa kitongoji cha Koumassi wamesema milio ya risasi ilisita jana jioni na watu kadhaa walitoka nje ya nyumba zao, lakini watu wapatao wawili waliuwawa katika ufyatulianaji wa risasi.

Mbali na mapigano kadhaa katika kitongoji cha Adjame, kilicho karibu na eneo la katikati la biashara mjini Abidjan, mapigano mengi yamekuwa yakitokea katika kitongoji cha Abobo kaskazini mwa mji huo, ambacho ni ngome ya kiongozi wa upinzani Alassane Ouattara, anayetambuliwa na jumuiya ya kimataifa kama mshindi halali wa uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba 28 mwaka jana.

Laurent Gbagbo
Rais wa Cote d'Ivoire Laurent GbagboPicha: Public Domain

Serikali ya Gbagbo imeanza kulipa mishahara wiki hii na imeyalenga matawi ya benki ya Societe Generale na BNP Paribas ili kuyataifisha, kama sehemu ya juhudi zake za kuusaidia uchumi usiporomoke. Benki ya Societe Generale imelaani vikali kuchukuliwa kwa tawi lake nchini humo pamoja na kutishwa kwa wafanyakazi wake.

Sambamba na hayo Marekani imewaonya raia wake dhidi ya kuitembelea Cote d'Ivoire. Wizara ya mambo ya ndani ya Marekani imewataka Wamarekani wajiepusha kwenda nchini humo hadi watakaposhauriwa kufanya hivyo. Imesema huku shinikizo dhidi ya Gbgabo likizidi, ukatili dhidi ya raia wa nchi za magharibi, wakiwemo Wamarekani, unaonekana kuongezeka. Inatarajia uchumi wa Cote d'Ivoire kuanguka, uhaba mkubwa wa nishati, chakula na mahitaji mengine, pamoja na mfumuko wa bei, mambo ambayo huenda yakasababisha hali ngumu kimaisha na kuzuka machafuko na uhalifu.

Wakati huo huo waasi kaskazini mwa Cote d'Ivoire wanasema mamilioni ya wakaazi wa eneo hilo wamekatiwa maji na umeme kwa kumuunga mkono Ouattara. Taarifa ya kampuni ya kitaifa ya umeme inasema wanaume waliokuwa na silaha walikatiza huduma za umeme Jumatatu wiki hii.

Kampuni hiyo imekuwa chini ya usimamizi wa rais Gbgabo aliyeitaifisha baada ya Umoja wa Mataifa kumtambua Ouattara kama mshindi wa uchaguzi wa Novemba mwaka jana.

Kwa upande mwingine matangazo ya radio ya BBC na Radio France International, RFI, hayakusika hewani hapo jana. Shirika la utangazaji la BBC limesema kwenye tovuti yake kuwa Laurent Gbagbo amekanusha kuchukua hatua dhidi ya vituo hivyo na halifahamu kwa nini matangazo yake yalisita. Gbagbo anavilaumu vyombo vya habari vya kimataifa kwa kuiyumbisha Cote d'Ivoire.

UN Sicherheitsrat Kongo
Alain Le RoyPicha: AP

Kwa upande mwingine, Umoja wa Mataifa umekiri ulifanya makosa kuishutumu Belarus kwa kuipelekea Cote d'Ivoire helikopta za kivita. Kiongozi wa tume ya kulinda amani ya umoja huo, Alain Le Roy, amewaambia waandishi wa habari jana mjini New York Marekani kuwa aliomba radhi kwa serikali ya Belarus kwa niaba ya Umoja wa Mataifa kwa ripoti hiyo ambayo haikuwa sahihi.

Jumapili wiki hii ofisi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon iliripoti kuwa helikopta moja ilikuwa imewasili Abidjan na kwamba helikopta zaidi zilikuwa zimepangwa kuwasili Jumatatu. Le Roy alisema taarifa hiyo ilitolewa na jopo huru la wataalamu linalosimamia vikwazo dhidi ya Cote d'Ivoire.

Mwandishi: Josephat Charo/APE/RTRE/AFPE

Mhariri: Saumu Yusuf