1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea kuchacha Yemen

Admin.WagnerD29 Julai 2015

Mapigano makali yameendelea kusini mwa Yemen ambako vikosi vinavyoiunga mkono serikali vimefaulu kuyadhibiti maeneo zaidi baada ya kuukomboa mji wa bandari wa Aden, kufuatia miezi minne ya mapigano na waasi wa Houthi.

https://p.dw.com/p/1G72l
Jemen Kämpfe um Aden
Picha: Reuters/Stringer

Duru za jeshi zimesema wapiganaji hao wamewafurusha waasi mjini Lahoum katika viunga vya kaskazini mwa Aden, kufuatia mapigano ambapo waasi 12 wameuawa. Duru za hospitali zimesema wapiganaji watatu wa kundi la Popular Resistance, wanaomuunga mkono rais wa Yemen Abedrabbo Mansour Hadi wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Mwandishi wa habari wa eneo hilo ameliambia shirika la habari la dpa kwamba wapiganaji hao wamefaulu kuyakomboa maeneo ya Jebel al-Zaytoun na al-Anad Triangle yaliyo karibu na kambi ya jeshi ya al-Anad, na huenda wakaiteka kambi hiyo katika saa chache zijazo.

Wakazi wamesema wapiganaji hao pia wamesonga mbele kuukaribia mji wa Huta, kiasi kilometa 20 kaskazini mwa kambi hiyo iliyoko katika mkoa wa kusini wa Lahj. Ndege za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zimefanya mashambulizi ya mabomu katika mkoa wa kaskazini wa Saada huku bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari likilupa karibu na hospitali ya Ath-Thawra mjini Sanaa na kusababisha majeruhi.

Usitishwaji mapigano haukuheshimiwa

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinaadamu, Stephen O'Brien, amesema jaribio la hivi punde kusitisha mapigano nchini Yemen ili kutoa fursa ya kusambaza misaada halikuheshimiwa na upande wowote ule katika mzozo huo na pande zote zimeshindwa kuheshimu sheria ya kimataifa."

Jemen Luftangriff auf Mocha
Mashambulizi ya kutokea angani MochaPicha: Reuters/Str

O'Brien amesema mpango wa kuwafikia watu milioni tatu na misaada uko tayari kuanza ikiwa tu mapigano yatakoma. Mkuu huyo amelihutubia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana na kurejea tena wito wa kusitisha mapigano bila masharti katika mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa kati ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabaia na waasi wa Houthi. Usitishwaji mapigano wa siku tano uliotangazwa siku ya Jumapili na muungano huo ulisambaratika haraka mapema Jumatatu wiki hii.

"Lazima tuongeze juhudi zetu maradufu kuafikia makubaliano ya kusitisha mapigano yatakayoheshimiwa na pande zote, na kuwafikia watu wote wenye mahitaji ya msingi, na kwa haraka kutoa muda na fursa ya kutafuta usitishwaji mapigano wa kudumu na suluhisho la kisiasa.

O'Brien ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufikia Ijumaa iliyopita vituo vya afya nchini Yemen vilikuwa vimeripoti vifo zaidi ya 4,000 vinavyohusiana na mzozo unaondelea. Amesema atakwenda Yemen Agosti 9.

Balozi wa Yemen katika Umoja wa Mataifa Khaled Alyaemany ameikaribisha ziara hiyo na kuongeza kusema, "Nawahimiza wanachama wa baraza la usalama kuwashinikiza zaidi Wahouthi. Nafikiri mapinduzi yanaweza kushindwa kwa ari ya jumuiya ya kimataifa kuliunga mkono azimio nambari 2216."

Wapiganaji tiifu wajiunge na majeshi

Wakati haya yakiarifiwa serikali ya Yemen iliyo uhamishoni nchini Saudi Arabia imetoa agizo kwa wanamgambo wanaopigana upande wa wanajeshi tiifu dhidi ya waasi wa Houthi wajiunge na majeshi ya nchi hiyo. Baraza kuu la ulinzi lililokutana jana mjini Riyadh liliamua kuwajumuisha wapiganaji wa kundi la Popular Resistance katika vikosi vya majeshi na vyombo vya usalama vya Yemen.

Mkutano huo, ulioongozwa na rais Abedrabbo Mansour Hadi, ulipitisha uamuzi huo kuwazawadi wapiganaji hao kwa mchango wao muhimu wa kishujaa katika kuilinda nchi yao.

Mwandishi:Josephat Charo/ape/dpae/afpe

Mhariri:Iddi Sessanga