1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano makali mjini Abidjan

4 Aprili 2011
https://p.dw.com/p/RFHn
Wapiganaji watiifu kwa Alassane Ouattara wakijiandaa kuuhujumu mji mkuu Abidjan.Picha: picture alliance / dpa

Wanajeshi wanaomuunga mkono Alassane Ouattara anayetambuliwa kimataifa kuwa rais halali wa Cote d´Ivoire wameanza hujuma mpya kwa lengo la kumuondoa madarakani Laurent Gbagbo kutoka ngome yake ya mwisho. Gbagbo pamoja na mashambulizi hayo bado anakataa kun´goka madarakani, akishikilia kwamba Ouattara siye mshindi wa uchaguzi wa Novemba mwaka jana bali aliyeshinda ni yeye binafsi, ikiwa ni kinyume na matokeo yaliotangazwa naTume ya uchaguzi.

Wakati mgogoro huo ukipamba moto, Ufaransa imetuma wanajeshi wengine zaidi katiaka taifa hilo la Afrika magharibi, kwa kile ilichosema ni kuwalinda raia.

Milio mizito ya mizinga na makombora na miripuko ilisikika mchana wa leo .Kamanda wa wapiganaji wanaomuunga mkono Ouattara, Issiaka Ouattara maarufu kwa jina la " wattao" aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba ana wapiganaji 4,000 pamoja na wengine 5,000 ambao tayari wameingia Abidjan. Akiongeza itachukua muda wa saa 48 kumaliza kile alichokiita safisha safisha mjini humo.

Baada ya kusonga mbele kuelekea mji mkuu bila ya upinzani wowote, wapiganaji wanaomuunga mkono Ouattara wamekumbana na upinazani mkali kutoka kwa majeshi ya Gbagbo katika eneo linaloizunguka Ikulu na stesheni ya televisheni ya taifa.

Kutokana na siku kadhaa za mapigano wakaazi wa mji mkuu wanazidi kuingiwa na hofu, na leo walionekana wakihaaha kutafuta chakula na maji, baada ya kuzuiwa majumbani kwa sababu ya mapigano.

Akizungumza hapo jana , waziri mkuu wa Ouattara ambaye pia ni waziri wa ulinzi Guillaume Soro alisema mkakati ulikua ni kwanza kuuzingira mji mkuu na kupata taarifa juu ya mahala walipojizatiti wanajeshi wa Gbagbo, kabla ya kuanza mashambulizi makali. Alisema sasa wakati ni muwafaka kuanza kazi hiyo.

Leo Ufaransa mkoloni wa zamani wa Cote d´Ivoire imesema inatuma wanajeshi 150 wa ziada kuwalinda raia na kuifanya idadi ya wanajeshi wake walioko nchini humo kufikia 1,650.Ufaransa pia ina raia wake 12.000 Cote dÌvoire na imeanza zorzi la kuwahamisha. pia wanajeshi wa ufaransa wanaudhibiti uwanja wa ndege wa Abidjan huku wakipiga pia doria katika mitaa ya mji mkuu huo.Inaaminiwa wapiganaji wa Ouattara wanaweza kukamilisha lengo lao la kumuangusha kabisa Gbagbo mapema, kutokana na ripoti kwamba wanajeshi kadhaa wa Gbagbo wamebadili upande wakijiunga na wapiganaji hao.

Mwandishi:Mohamed Abdul-Rahman /RTR

Mhariri :Saumu Mwasimba