Mapato ya Kenya ya zao la chai yapungua. | Masuala ya Jamii | DW | 23.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Mapato ya Kenya ya zao la chai yapungua.

Mnunuzi mkubwa Pakistan ageukia zaidi nchi nyengine.

default

Mkulima akichuma chai katika shamba moja huko Limuru nchini Kenya.

Chai ni zao lililokuwa likiipatia Kenya pato kubwa, lakini hata kabla ya mtumiaji mkubwa wa Chai-Pakistan, haikuingia kwenye makubaliano huru ya kibiashara na saba kati ya majirani zake barani Asia, tayari kiwanda cha Chai kilikua kikinawiri nchini Kenya.Lakini sasa kutokana na kuzidi kwa mashindano kwenye masoko, kiwango cha chai inayouzwa na Kenya kimepungua.

Miaka mitano iliopita, nchi hii ya kilimo katika kanda ya Afrika mashariki yenye wakaazi 35 milioni , ikisafirisha hadi asili mia 85 ya matumizi ya chai ya Pakistan. Lakini sasa kutokana na kuongezeka mashindano katika soko la dunia kiwango hicho cha Kenya kimeshuka hadi asili mia 65.Ikiagiza kiasi ya kilo 170 milioni za chai kwa mwaka, Pakistan ni mnunuzi mkubwa kabisa wa zao hilo duniani.

Kiwanda cha chai nchini Kenya, kingependelea kurudi nyuma miaka saba iliopita pale ubalozi wa Pakistan mjini Nairobi ulipojaribu kuunda eneo la biashara huru (Free Trade Area) pamoja na Kenya, taifa lililokua usoni kiuchumi katika Afrika mashariki-pendekezo ambalo halikufanyiwa kazi tangu wakati huo.

Kenya imelikataa ombi la Pakistan la kuwa na eneo la biashara huru, kwa sababu makubaliano ya aina hiyo yatapin´gana na yale ya kutolipishana ushuru miongoni mwa nchi wanachama wa Soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika (COMESA), pamoja na Jumuiya ya Afrika mashariki ambayo Kenya pia ni mwanachama.

Tarakimu rasmi za Bodi ya chai nchini Kenya (TBK) zinaashiria kwamba mapato na kiwango cha chai iliokua ikisafirishwa kwenda Pakistan yamepungua.Mnamo mwaka 2005 kwa mfano, wakati mapato yanayotokana na chai yalipoongezeka kwa mara ya mwisho panapohusika na fedha za kigeni, Pakistan iliagiza kilo 98 milioni za chai kwa gharama ya shilingi 12 bilioni za Kenya, sawa na dola 186 milioni za Marekani.

Miaka miwili baadae Kenya ilipokea Shilingi 10 bilioni kutoka Pakistan, pato lililoshuka kwa asili mia 20, iliposafirisha tu kilo 80 milioni za chai.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa utawala wa TBK Sicily Kariuki, nafasi ya Pakistan imechukuliwa na Misri na Uingereza katika robo mbili za kwanza za mawaka huu. Kwa hivi sasa anasema Bibi Karuki, Misri ianaongoza kawa kuagiza kilo 43 milioni, ikifuatiwa na Uingereza kilo 32 milioni na Pakistan inashika nafasi ya tatu kwa kuagiza kilo 25 milioni.

Kupungua kwa kiwango cha chai inayosafirishwa hadi Pakistan kwa hivyo kunatokana na kusita kwa Kenya kuafikiana na pendekezo la kua na eneo la biashara huru. Badala yake Pakistan imetiliana saini mkataba wa aina hiyo na mataifa mengine ya Asia, Bangladesh, Bhutan, India, Maldives, Nepal, na Sri Lanka. Tokea Janurai 2006 Pakistan na Sri Lanka taifa lenye kulima chai kwa wingi barani Asia zimeondoleana ushuru kwa bidhaa kadhaa zipatazo 206 zinazoingia Pakistan na Chai ni zao lilioko nafasi ya usoni.

Pakistan sasa imo katika kuzungumza Malawi na Rwanda ambapo huenda mataifa hayo yanayolima chai barani Afrika yakafunga mkataba na pakistan chini ya ule utaratibu wa eneo huru la biashara FTA. Bila shaka hilo, litahujumu zaidi nafasi ya Kenya kama msafirishaji mkubwa barani Afrika wa zao hilo la chai hadi Pakistan,

Kuimarika kwa ubora wa chai ya Rwanda na Malawi kwa upande mwengine, utakua mtihani mwengine kwa Kenya katika biashara ya zao hilo.

 • Tarehe 23.09.2008
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/FNY5
 • Tarehe 23.09.2008
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/FNY5