1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yazuka Tripoli

17 Novemba 2013

Kumezuka mapambano Jumamosi(16.11.2013) katika mji mkuu wa Libya wakati wanajeshi na wanamgambo wenye mafungamano na serikali walipojaribu kuirudisha kambi moja iliokaliwa kwa mabavu na wapiganaji wenye silaha.

https://p.dw.com/p/1AIsD
Maandamano ya kutaka wanamgambo waondoke Tripoli (15.11.2013)
Maandamano ya kutaka wanamgambo waondoke Tripoli (15.11.2013)Picha: Reuters

Mpiganaji wa upande wa serikali amesema mwenzao mmoja ameuwawa kwa kupigwa risasi katika mapambano hayo kwenye kitongoji cha Tajoura mashariki ya Tripoli. Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali LANA wapiganaji wanane wanaounga mkono serikali wamejeruhiwa.Wanajeshi na wanamgambo wenye kuiunga mkono serikali walikuwa wakijaribu kurudisha udhibiti katika kambi iliokuwa imeshambuliwa Ijumaa jioni na wanamgambo waliokuwa wametokea katika mji ulioko jirani wa Misrata.

Kamanda wa jeshi katika kambi hiyo Kanali Musbah al Hama amelimbia shirika la habari la LANA kwamba wanamgambo kutoka mji wa mashariki wa Misrata waliishambulia tena kambi hiyo alfajiri ya Jumamosi.Al-Hama amesema wanamgambo hao baadae waliondoka kwenye kambi hiyo na kuchukuwa silaha nyingi na risasi na hivi sasa wako ukingoni mwa mji huo mkuu.

Tripoli iko hatarini

Mji mkuu wa Tripoli uko katika hatari ya kutumbukia kwenye vurugu baada ya wanamgambo wengine kutoka Misrata hapo Ijumaa kuwafyetulia risasi waandamanaji waliokuwa wakidai kuvunjwa kwa makundi ya wapiganaji yalioko kinyume na sheria na kuuwa watu 43 na kujeruhi wengine 400.Maduka mengi katika mji mkuu huo yamefungwa Jumamosi na serikali imetangaza siku tatu za maombolezo.

Waziri Mkuu wa Libya Ali Zidan pia ameonya hapo Jumamosi juu ya majaribio ya wanamgambo kutoka nje ya Tripoli kuingia katika mji mkuu huo kwa kusema kwamba jambo hilo litakuja kusababisha umwagaji mkubwa wa damu.

Muadamanaji aondolewa baada ya kujeruhiwa kufuatia mashambilizi ya wanamgmabo dhidi ya waandamanaji mjini Tripoli . (15.11.2013)
Muadamanaji aondolewa baada ya kujeruhiwa kufuatia mashambilizi ya wanamgmabo dhidi ya waandamanaji mjini Tripoli . (15.11.2013)Picha: picture-alliance/AP Photo

Kikosi cha Usaidizi cha Umoja wa Mataifa nchini Libya kimewataka Walibya kuchukuwa hatua za kuvumiliana na kutatuwa tafauti zao kwa njia ya amani.Kikosi hicho kimesema katika taarifa kwamba kinalaani vikali ghasia zilizozuka Tripoli na kusababisha maafa miongoni mwa raia na kutaka kusitishwa mara moja kwa uhasama.

Tokea kuangushwa kwa dikteta Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011 mamia ya wanamgambo wengi wao wakiwa kwenye orodha ya malipo ya serikali wamekuwa wakijifanyia wanavyotaka nchini Libya na kuunda kanda za mamlaka yao,kukataa mamlaka za serikali na kufanya mashambulizi ya umwagaji damu.Serikali ya Libya imeshindwa kuwalazimisha kujiunga na jeshi la polisi na lile la ulinzi lililo dhaifu ambalo serikali imekuwa mbioni kuliunda huku kukiwa na hali ya kutoridhika ya wananchi ya kutokuwepo kwa usalama nchini humo.Hususan mienendo ya wanamgambo wa Misrata imechemsha ghadhabu ya wananchi.

Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan.
Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan.Picha: Reuters

Hali ya usalama imeimarishwa Jumamosi hususan katika mji wa Tripoli wakati mazishi yakifanyika kwa wale waliouwawa Ijumaa. Wanamgambo wenye mafungamano na serikali na wakaazi wenye silaha waliweka vizuizi vya ukaguzi katika mji mzima wa Tripoli na njia kuu za kuingilia katika mji huo kuwazuwiya wapiganaji kuingia mjini humo na kuvilinda vitongoji vyao dhidi ya ghasia zaidi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Bruce Amani