1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yatishia kuvunja mazungumzo ya Geneva

-12 Juni 2013

Wanaharakati nchini Syria wanasema waasi wameshambulia kijiji kimoja katika eneo la mashariki na kuua watu kadhaa kutoka madhehebu ya shia,wengi wao wakiwa ni wanaounga mkono majeshi ya serikali

https://p.dw.com/p/18oAJ
Kifaru cha jeshi la Syria,mjini Qusayr katika mkoa wa Homs
Kifaru cha jeshi la Syria,mjini Qusayr katika mkoa wa HomsPicha: Str/AFP/Getty Images

Kundi la waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema kiasi ya watu 60 wameuwawa katika kijiji cha Hatia katika mkoa wa Deir el-Zour siku ya Jumanne.

Kwa mujibu wa wanaharakati wa kundi linalofuatilia haki za binadamu lenye makao yake London, mashambulio ya waasi katika kijiji hicho ni ulipizaji kisiasi dhidi ya shambulio lililofanywa na washia kutoka kijiji hicho lililosababisha waasi wanne kuuwawa.Wakaazi wengi wa kijiji hicho wamelazimika kutorokea kijiji kilicho karibu cha Jafra.

Mapambano hayo yamekuja wiki moja baada ya wanajeshi wa Serikali wakisaidiwa na Hezbollah kuuteka mji muhimu wa Qusair karibu na mpaka wa Lebanon.

Mawaziri wa nje wa Marekani John Kerry na Laurent Fabius wa Ufaransa
Mawaziri wa nje wa Marekani John Kerry na Laurent Fabius wa UfaransaPicha: AFP/Getty Images

Hatma ya kikao cha Geneva

Upande mwingine Ufaransa imesema kwamba waasi wa Syria huenda wakagoma kushiriki katika mazungumzo muhimu ya kusaka suluhu na serikali ya rais Bashar al -Assad ikiwa wanajeshi wa serikali hiyo wataendelea na hatua yao ya kusogea katika ngome ya waasi ya Aleppo.

Wanajeshi hao wa serikali wanajikusanya wakiukaribia mji huo wakijindaa kushambulia na kuuteka mji huo na kujiimarisha tena kufuatia kuongezeka kwa mapigano kutokana na jeshi la Assad kupata uungaji mkono wa kundi la Hezbollah.Akizungumza na na kituo cha televisheni cha France 2 waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema ni lazima wanajeshi wa Assad wazuiwe kusonga mbele ili kuleta usawa katika vita hivyo la sivyo huenda hakutokuweko mazungumzo ya Geneva kwasababu ni wazi waasi hawatokubali kushiriki.

Wasiwasi juu ya kuwahami waasi

Marekani na Urusi zinajaribu kuwaleta pamoja serikali ya Assad na wapinzani wake katika kikao cha mwezi Julai mjini Geneva lakini bado nchi hizo mbili zimo katika hali ya kutofautiana juu ya masuala kadhaa kabla hata mazungumzo hayo hayajaanza.Ufarsana ni miongoni mwa nchi za magharibi pamoja na Marekani na Uingereza ambazo zinasema rais Assad hana tena uhalali wa kuliongoza taifa hilo ingawa viongozi wa nchi hizo hawajafikia uamuzi wa kuwapa waasi silaha kutokana na hofu ya kuwaingiza madarakani wapiganaji wa siasa kali za kiislamu.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Fabius amesema nchi yake itaheshimu makubaliano ya Umoja wa Ulaya ya kutowapa silaha waasi kabla ya Agosti 1 lakini amesema amezungumza na mwenzake wa Marekani John Kerry hapo jana juu ya suala hilo.Aifdha ametilia mkazo kwamba hakuna mtu yoyote inayojadili juu ya kupeleka kikosi nchini Syria lakini waasi lazima wawezeshwe kujilinda dhidi ya jeshi la Serikali linalotumia ndege na silaha nzito nzito na kudaiwa pia kutumia silaha za kemikali.

Kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya juu ya Syria mjini 27.05.2013
Kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya juu ya Syria mjini 27.05.2013Picha: picture alliance/AP Photo

Huku hayo yakijiri kiongozi wa shughuli za kuweka amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous ameiomba Austria muda zaidi ili umoja huo upate nafasi ya kuandaa ujumbe utakaochukuwa nafasi inayoachwa na kikosi cha Austria kinachojiandaa kuondoka katika milima ya Golan ambalo ni eneo la usalama kati ya Syria na Israel.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman