1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yaendelea kwenye kambi ya Nahr al Bared

Josephat Charo13 Julai 2007

Wanajeshi wa Lebanon wameendelea kuishambulia kambi ya wakimbizi wa kipalestina ya Nahr al Bared kaskazini mwa hiyo hii leo. Wakati huo huo wanamgambo wa kundi la Fatah al Islam walio ndani ya kambi hiyo wamekabiliana na wanajeshi hao kwenye mapambano makali.

https://p.dw.com/p/CHAx
Wanajeshi wa Lebanon wakielekea kwenye kambi ya Nahr al Bared
Wanajeshi wa Lebanon wakielekea kwenye kambi ya Nahr al BaredPicha: AP

Wanajeshi wa Lebanon wameyashambulia kwa mabomu maeneo yanayotumiwa na wanamgambo kuvurumishia maroketi kwenye kambi ya Nahr al Bared kaskazini mwa Lebanon, huku idadi ya wanajeshi waliouwawa kwenye uvamizi wa kambi hiyo ikikaribia kufikia 100 katika kipindi cha wiki nane.

Wanamgambo wa kundi la Fatah al Islam wamevurumisha maroketi 11 aina ya Kyatusha. Mengi yao yameanguka kwenye mashamba yaliyo kilomita kadhaa kaskazini mashariki na kusini mwa kambi ya Nahr al Bared. Hakuna aliyeuwawa wala kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo ya maroketi.

Mapigano yalianza mnamo tarehe 20 mwezi Mei mwaka huu wakati wanamgambo wa kiislamu walipofanya mashambulio kadhaa dhidi ya wanajeshi na kuwaua wanajeshi 27 katika maeneo yanayoizunguka kambi ya wakimbizi ya Nahr al Bared na katika mji wa bandari ulio karibu wa Tripoli.

Serikali mjini Beirut imeapa kuwachakaza wanamgambo hao wa kundi la Fatah al Islam wanaopata ushawishi kutoka kwa kundi la Al Qaeda. Mwanajeshi wa nane ameuwawa hii leo kwenye mapambano baina ya wanajeshi na wanamgambo walio ndani ya kambi hiyo ya wakimbizi wa kipalestina iliyozingirwa na wanajeshi wa Lebanon.

Msemaji wa jeshi la Lebanon, amethibitisha kuuwawa kwa mwanajeshi huyo. Aidha amesema wanajeshi wanaendelea na msako wa nyumba kwa nyumba pole pole na kwa uangalifu mkubwa kuelekea maeneo ya wanamgambo. Amesema wahandisi wa jeshi wanashirikiana na wanajeshi katika operesheni hiyo.

Mbali na mashambulio ya mabomu, kumekuwa na ufyatulianaji wa risasi baina ya vikosi vya Lebanon na wanamgambo wa kiislamu. Mapigano yalisita wakati wa sala ya Ijumaa lakini yakaanza tena muda mfupi baadaye. Shughuli za uokozi zilikwama tangu juzi Jumatano wakati wafanyikazi wa kutoa misaada walipokuwa wakijaribu kuwaokoa watoto takriban 45 na wanawake 20 jamaa za wapiganaji walioshindwa kufika kituoni walikotakiwa wakusanyike.

Sambamba na hayo wanasiasa wanaohasimiana wa Lebanon hapo kesho wataanza mkutano wa siku mbili unaodhaminiwa na Ufaransa karibu na mji mkuu Paris. Mkutano huo hata hivyo hautarajiwi kuleta ufanisi mkubwa katika kuutanzua mgogoro wa kisiasa unaotishia kuitumbukiza Lebanon kwenye machafuko.

Ibrahim Kanaan, muwakilishi wa kiongozi wa kikristo wa upinzani nchini Lebanon, Michel Aoun, amesema mkutano wa Paris si suluhisho la mwisho bali ni chanzo cha kuanza mkakati mpya na utajenga uaminifu na kutoa mwanya mazungumzo yaanze tena mjini Beirut.

Wizara ya mashauri ya kigeni ya Ufaransa imesema mkutano huo utafanyika kwa siku mbili badala ya tatu kama ilivyokuwa imepengwa hapo awali kwa sababu mwenyekiti wa mkutano huo, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa, Bernard Kouchner, ana shughuli nyingine.