Mapambano makali yazuka Bangkok
15 Mei 2010Wito huo umetolewa baada ya waandamanaji 10 kuuawa katika mapambano yaliyozuka kati ya wanajeshi na waandamanaji wa upande wa upinzani, wanaojulikana kama "mashati mekundu" pia. Ripoti zinasema jumla ya wale waliouawa, sasa imefikia 16 na zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa, miongoni mwao wakiwemo raia watatu wa kigeni. Msemaji wa Ban Ki-moon amezihimiza pande zote mbili yaani serikali na waandamanaji hao warejee katika meza ya mazungumzo.
Machafuko yameendelea katika mji mkuu Bangkok, kwa siku ya tatu leo, tangu yalipoanza Alhamisi. Wanajeshi waliwashambulia waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe na mabomu ya petroli barabarani, baada ya wanajeshi kusonga mbele katika eneo la kibiashara la Rath Chap Rasong. Wanajeshi hao wamelivamia eneo hilo kwa azma ya kuzima maandamano ya upinzani yanayoendelea tangu miezi miwili hivi sasa. Waandamanaji hao wanaipinga serikali ya Waziri Mkuu Abhist Vejjajiva. Barabara zinazoelekea katika eneo la biashara zimefungwa, ili kuzuia waandamanaji kuingia katika maeneo hayo. Hali ya hatari imetangazwa katika maeneo mengi nchini humo ikiwa ni pamoja na mji mkuu Bangkok.
Mwandishi:Munira Muhammad/IPS
IMhariri:P.Martin