1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maonyesho makubwa ya tekinolojia CeBIT

Abdu Said Mtullya2 Machi 2010

Maonyesho makubwa ya tekinolojia yanayofanyika kila mwaka nchini Ujerumani yanaendelea mjini Hannover.

https://p.dw.com/p/MHzh
Maonyesho ya tekinolojia yameanza mjini Hannover lakini idadi ya makampuni na washabiki inatarajiwa kupungua.Picha: AP

Maonyesho ya tekinolojia makubwa kuliko mengine yote duniani yanaendelea katika mji wa Hannover,kaskazini magharibi mwa Ujerumani.Hata hivyo, wachunguzi wanasema mwaka huu vilevile maonyesho hayo yamepungukiwa na washiriki.

Makampuni 4157 kutoka nchi 68 yanashiriki kwa kuonyesha bidhaa mpya kwa muda wa siku tano. Idadi hiyo ni ya kiwango cha chini ambacho hakijawahi kufikiwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Pamoja na kutambulisha bidhaa za aina mpya, waandalizi wa maonyesho pia wanakabiliwa na jukumu la kujaribu kurejesha hadhi ya hapo awali ya maonyesho hayo.Hata hivyo,mwenyekiti wa kampuni ya maonyesho, Wolfram von Fritsch, amesema maonyesho hayo bado ni muhimu leo vilevile.

Maonyesho hayo,yanayofanyika chini ya kauli mbiu inayosema dunia iliyoungana, yalifunguliwa rasmi na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na waziri mkuu wa Uhispania, Zapatero.Uhispania ndiyo nchi mshirika katika maonyesho ya mwaka huu.

Kansela Merkel na waziri mkuu Zapatero pia wamesisitiza umuhimu wa sekta ya tekinolojia katika mustakabal wa Ulaya.Na kwa ajili hiyo, bibi Merkel ametoa mwito wa kuweka kipaumbele juu ya tekinolojia katika uchumi wa Ujerumani.

Amesema serikali ya Ujerumani itawasilisha mkakati mpya utakaonyesha katika kipindi cha kiangazi, jinsi itakavyofungamanisha maendeleo katika sekta ya taaluma ya kompyuta na sekta nyingine za viwanda vya jadi,kama vile vya magari na vya kemikali.

Bibi Merkel amesema Ujerumani itachukua hatua zaidi ili sekta ya tekinolojia ipatiwe nafuu zaidi za kodi, lakini bibi Merkel amepinga wazo la kuanzisha wizara ya internet katika baraza la mawaziri.

Kwenye maonyesho ya mwaka huu,kampuni zinatambulisha simu za mkononi za aina mpya, zinazoweza kufungua milango, zana zinazopunguza matumizi ya nishati na zana zinazoweza kupima mienendo ya midomo na kuibadili miendendo hiyo kuwa mapigo ya muziki.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, akifuatana na mgeni wake, waziri mkuu Zapatero wa Uhispania, waliyatembelea mabanda ya makampuni maaruf, IBM, Microsoft na Telefonica.

Maalfu ya wananchi leo wameanza kuyatembelea maonyesho hayo.Hata hivyo,wachunguzi wanatarajia kupungua kwa idadi ya washabiki.

Mwandishi/ Wenkel Rolf/ZA

Imetasfiriwa na Mtullya Abdu.

Mhariri: Miraji Othman