1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yashinikizwa na NATO kushiriki kusini mwa Afghanistan

Mtullya, Abdu Said11 Machi 2008

Ujerumani yapinga kupeleka majeshi kusini mwa Afghanistan.

https://p.dw.com/p/DMmw
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ziarani AfghanistanPicha: AP




Katibu Mkuu wa mfungamano wa kijeshi wa NATO Jaap de Hoop Scheffer ameitaka  Ujerumani ishiriki katika jukumu la kulinda amani kusini mwa Afghanistan -sehemu inayokabiliwa na mashambulio ya mara kwa mara lakini Ujerumani imesema haitapeleka majeshi yake katika  sehemu  hiyo.

Hayo anasema mwandishi wetu Sybille Golte katika maoni yake.


Hakuna mtu  anaetaka  kusimama mahala anaposimama Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuhusiana na suala la Afghanistan.Kila anapokutaka na   viongozi wa nchi zingine za NATO kansela huyo anakabiliwa na shinikizo la kutaka majeshi ya Ujerumani pia yashiriki katika jukuimu la kulinda amani kusini  mwa  Afghnaistan sehemu inayoripuka  mara kwa mara.Shinikizo hilo limerudiwa   kwa mara nyingine na katibu Mkuu wa  jumuiya ya kijeshi ya NATO  Jaap de Hoop Scheffer alipokutana na kiongozi huyo wa Ujerumani mjini Berlin.

Ni jambo linaloeleweka kwa wanachama wengine wa NATO kuitaka Ujerumani nayo ipeleke majeshi kusini mwa Afghastan. Na kama alivyolalamika katibu mkuu wa mfungamano wa NATO, Scheffer, siyo sawa kwa baadhi ya nchi kushiriki katika mapambano nchini Afghanistan wakati zingine zinashughulikia mambo ya ugavi tu.

Lakini Kansela Merkel hataki majeshi ya nchi yake yashiriki kusini mwa Afghanistan.

Kwanza anatambua kwamba hataungwa mkono bungeni. Sababu inafahamika wazi, kuwa idadi kubwa ya wananchi wa Ujerumani wanapinga  zoezi lote la kupeleka majeshi nchini Afghanistan achilia mbali kuweka majeshi kusini mwa nchi hiyo.

Idadi ya wajerumani wanaopinga jukumu la Afghanistan inaongezeka, kwa kadri habari zinavyozidi kuwa mbaya kutoka nchi hiyo.

Badala ya kupeleka majeshi kusini mwa Afghanistan Kansela wa Ujerumani anasisitiza mkakati wa kutangamanisha misaada ya maendeleo na ya kijeshi. Anaamini mkakati huo utakuwa na ufanisi mkubwa zaidi katika kuwashinda mataliban. Ni wazo zuri, lakini majeshi ya nchi zingine yanakabiliana na matilaban kwenye uwanja wa mapambano.

Huo ni mtanziko mkubwa kwa Ujerumani.

Jee Kansela wa Ujerumani ataamua vipi?


Asilani hatapata idadi kubwa ya wabunge wa kumwuunga mkono- lakini wakati huo   huo shinikizo la wanachama wengine wa  NATO linaimarika.

Viongozi wa nchi na serikali wa nchi za mfungamano huo wanatarajiwa kukutana  mwezi ujao mjini Bukarest-Rumania. Bila shaka Kansela Merkel atakabiliwa tena na suala la Afghanistan.

Na mjadala unakuwa mkali zaidi baada ya Umoja wa Mataifa kutoa takwimu juu ya matukio ya nchi hiyo. Umoja wa Mataifa umesema umwagaji damu mwaka jana ulifikia kiwango kisichokuwa na mithili tokea majeshi ya Marekani yaivamie nchi hiyo ,miaka saba iliyopita.

Suala la kubeba mzigo wa Afghanistan katika msingi wa usawa  miongoni mwa nchi wanachama wa NATO ni sehemu tu ya tatizo. Ukweli ni kwamba ,mkakati ambao umekuwa unatumika hadi sasa bado haujathibiti kuwa wa mafanikio.

Hivyo basi suluhisho litapatikana katika mkakati mujarab.