1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barack afanikiwa kutekeleza lengo lake.

Abdu Said Mtullya25 Machi 2009
https://p.dw.com/p/HJIL
Picha: picture-alliance / dpa

Kiongozi  wa chama cha Leba nchini Israel  Ehud Barack amefanikiwa kutekeleza lengo lake. Chama chake kitaingia katika serikali ya mseto na chama  cha kihafidhina -Likud,cha waziri mkuu  mteule, Benjamin Netanyahu.

Chama cha Leba kimemsaidia kiongozi wa chama  cha Likud kuingia madarakani.

Kiongozi wa chama cha Leba Ehud Barack alipata   asilimia 58 ya kura zilizomuunga mkono. 

Barack amefanikiwa kutekeleza shabaha yake baada   ya mazungumzo  ya  usiku kucha na kiongozi wa  chama cha Likud, Netanyahu.


Chama  cha Leba ambacho kwa miaka mingi kilikuwa chama cha mstari wa mbele,mwasisi wa nchi na kiongozi wa serikali ya kwanza ya Israel kilimaliza katika nafasi ya  nne katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kiliambulia viti 13 katika bunge lenye viti 120.

Kujiunga  na serikali ya mseto hakutazuia kuanguka kwa chama hicho bali hatua hiyo itaharakisha  kuanguka huko.

Kwa wanachama wengi wa chama hicho,Barack   amechukua hatua hiyo ili kutekeleza maslahi yake binafsi.

Ni wazi kwamba bwana Barack hatakiri hayo, kwani akifanya hivyo atakuwa anajisuta mwenyewe . Wakati  wa uchaguzi  alizungumzia juu ya kuingia katika  upinzani.Lakini sasa amegeuza kauli.

Amesema kuwa  hamwogopi Netanyahu na kwamba   ataleta  urari katika mizani ya serikali dhidi ya sera  zote za mwelekeo mkali wa kulia.

Amehoji kuwa kama mshiriki katika serikali ya mseto  ataweza  kufikia mengi zaidi kuliko kuwa katika upinzani na viti 13 tu.

Yumkini inaweza kuwa hivyo lakini swali ni,  Ehud Barack  anaweza  kutimiza na kupata nini katika serikali kama hiyo.? Yaani serikali itakayoongozwa na waziri mkuu aliesema katika kampeni za uchaguzi kwamba hana haja kubwa ya kuanzisha tena mazungumzo ya kuleta amani.

Atapata nini katika serikali ambapo waziri wa mambo ya nje anatazamiwa  kuwa mtu anaeitwa Avigdor Liebermann mwanasiasa  mwenye itikadi kali za mrengo wa kulia-mwanasiasa alietishia kuliteketeza   bwawa  la Asuan nchini Misri.Mwanasiasa huyo  anawaona waisraeli wenye nasaba ya kiarabu kuwa maadui wa nchi na ambae angetaka kuona Iran  ikishambuliwa leo badala ya kesho.

Matatizo na migongano imeshajenga mizizi  ndani na nje ya Israel.

Tayari pana  sauti kutoka Umoja wa Ulaya zinazosema kuwa haitawezekana kushirikiana na serikali hiyo ya mrengo mkali wa kulia.Pana wasi  wasi nchini Marekani vilevile.Serikali hiyo pia itaimarisha mtazamo wa waarabu ambao wakati wote  wamekuwa wanasema kuwa Israel haitaki amani.

Kwa kuingia katika serikali ya mseto na chama cha Likud Ehud Barack amerudisha nyuma matumaini ya amani.