1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya2 Juni 2009

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya ajali ya ndege na juu ya kufilisika kwa GM.

https://p.dw.com/p/I28F
Ndege ya shirika la Ufaransa kabla ya kupatwa na ajali.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya ajali ya ndege ya shirika la Ufaransa-Air France na juu ya
kampuni ya magari ya Marekani iliyofilisika.

Gazeti la Berliner Zeitung linasema katika maoni yake kwamba mkasa wa kampuni ya magari ya Marekani GM unaashiria mwisho wa enzi ya nguzo mojawapo kuu ya sekta ya viwanda nchini Marekani.Mhariri wa gazeti hilo pia anatilia maanani hatua iliyochukuliwa na utawala wa rais Obama.

Gazeti linasema rais Barack Obama amefanya jaribio lisilokuwa na mithili katika mfumo wa uchumi wa nchi yake- mfumo huru. Utawala wa Marekani utakuwa mmiliki wa kampuni ya GM na hivyo kuipa kampuni hiyo pumzi ya uhai. Lakini gazeti linasema kwa kuchukua hatua hiyo rais Obama anacheza patapotea ya hatari kisiasa.

Mhariri anatahadhirisha kuwa, ikiwa GM itashindwa kuwa kampuni yenye faida, mnamo kipindi kifupi kijacho,mzigo wa lawama utabebwa na rais Obama.

Gazeti la Mannheimer Morgen linazungumzia juu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Gazeti hilo linalalamika kwamba hadi sasa rais Obama hajakuwa tayari kuchukua hatua ndefu katika suala la upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Marekani inakataa kupunguza kwa asilimia 25 kiwango cha hewa chafu- yaani ya kaboni.Gazeti la Mannheimer linasema kwa kufanya hivyo Marekani inatetea maslahi ya China vilevile. Mhariri anaeleza kuwa huenda Marekani na China zikasimama pamoja na kuzuia kufikiwa mapatano, kwenye mkutano juu ya mabadiliko ya hali ya hewa utakaofanyika mjini Copenhagen mnamo mwezi desemba.

Ndege ya abiria ya shirika la Ufaransa imepatwa na ajali ikiwa na watu 228 na mpaka sasa hazijapatikana habari za uhakika, juu ya nini hasa kilichosababisha ajali hiyo. Juu ya maafa hayo gazeti la Schwarzwälder Bote linakumbusha juu ya muujiza uliotokea kwenye mto wa Hudson nchini Marekani. Ndege ya abiria ilianguka katika mto huo na abiria 155 walinusurika.

Safari hii, sote tuna hofu, anasema mhariri wa gazeti hilo. Nini kimetokea,bado haijafahamika kwa uhakika. Hatahivyo mhariri huyo anatilia maanani kwamba mkasa huo umetokea katika dunia ya tekinolojia ya hali ya juu.

Mwandishi:A.Mtullya

Mhariri:M.Abdul-Rahman