1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said7 Mei 2008

Wahariri wa magazeti leo wanazungumzia juu ya kuapishwa rais mpya nchini Urusi na juu ya maafa nchini Mynmar.

https://p.dw.com/p/Dv22
Rais mpya wa Urusi D. Medvedev na waziri mkuu mpya V Putin.Picha: AP

Katika maoni  yao  wahariri  wa magazeti ya Ujerumani leo wanazingatia hasa masuala  ya nje.

Lakini wahariri hao pia  wanazungumzia juu ya  tatizo la watoto wanaokabiliwa na ugumu katika masomo yao nchini Ujerumani.Wengi wanahitaji msaada hata  baada ya kumaliza shule.

Gazeti  la WESTFÄLISCHER ANZEIGER linazungumzia  juu ya Urusi ambapo rais wa hadi  sasa Vladimir Putin leo  amekabidhi madaraka kwa rais mpya, Dimitry Medvedev.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema ,hata  kufikiria  tu  kwamba mabadiliko yanafanyika ni kupiga chuku. Anasema kinachotokea  ni  kwamba  rais huyo mpya anaingia ofisini kuenda kukalia kiti alichosogezewa na Putin. Lakini ukweli ni kuwa Putin ataendelea kushika hatamu za uongozi.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba warusi wanataka mtu kama Putin awe kiongozi wao.

Na kutokana  na hayo  itakuwa vigumu kwa rais mpya ,Medvedev kuingia madarakani  na kutekeleza sera zake.

Gazeti la RHEIN-NECKER ZEITUNG linamzungumzia  rais mwengine; Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ambae kwa sasa anaanguka katika umaaruf.

Kura za maoni  zinathibitisha  hayo. Lakini gazeti hilo linaeleza kuwa, kinachomfanya rais  Sarkozy aanguke katika kura za maoni ,siyo hasa siasa zake bali ni mitindo anayotumia katika kutekeleza siasa hizo. Mhariri anasema mara nyingi rais huyo anaonekana kuwa mwingi wa pupa.

Pamoja  na hayo kiongozi huyo anaonekana kuwa ametingwa na mambo mengi  katika maisha yake ya faragha.

Gazeti la  WESTFÄLISCHE NACHRICHTEN linazungumzia juu ya maafa yaliyotokea nchini Mynmar na jinsi utawala wa nchi hiyo unavyokabiliana na maafa hayo.

Mahariri wa gazeti  hilo anasema utawala huo umeonesha uzuzu usiosemeka.

Gazeti  linasema utawala wa Mynmar ulitumia vyombo vya habari kueneza propaganda  juu ya kura ya maoni badala  ya kuwaandaa wananchi ili waweze kuyakabili maafa yaliyosababishwa na kimbunga Nargis.

Mhariri anasema  wakati watawala hao walipokuwa wanaeendesha  propaganda ya kuimarisha  utawala  wao, kimbunga Nargis kimeendelea  kuleta maangamizi.


Gazeti  la WESTDEUTSCHE linaeleza wasiwasi  juu ya mfumo wa elimu nchini Ujerumani. Linatilia maanani kuwa theluthi moja ya watoto wa shule wanahitaji msaada  wa  masomo ya ziada. Juu ya  hayo  gazeti la WESTDEUTSCHE  linasema

katika  jitihada za  kuleta maguezi , baada ya  kuzembea  kwa muda mrefu shule  zimechukua  hatau nyingi kwa pamoja. Kwa mfano zimeanzisha mitihani ya pamoja  na  mitihani ya kuwahamasisha watoto-mhariri anasema hayo yote yamefanyika bila ya kubadili mpango wa masomo, bila ya kuongeza walimu na bila ya kupunguza idadi ya  watoto madarasani. Gazeti linasema badala ya kusaidia, mageuzi hayo yamegeuka  kuwa  shinikizo kwa watoto.

Na matokeo yake ni kwamba theluthi moja ya watoto  wanahitaji-tuishen,yaani msaada  maalum.