Maoni ya wahariri | Magazetini | DW | 19.07.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri

Mashirika ya serikali ya televisheni ARD na ZDF yamesimamisha matangazo ya mashindano ya mbio za baiskeli baada ya kufahamika kwamba mwanamichezo mwingine wa Ujerumani amegundulika kuwa ametumia madawa ya kuongeza nguvu. Wahariri wa magazeti, leo wanatoa maoni yao juu ya hatua hiyo.

Katika maoni yao wahariri hao pia wanazungumzia juu ya urari wa kazi aliyotimiza kansela Angela Merkel hadi sasa tokea aanze kuiongoza Ujerumani.

Mashindano ya mbio za baiskeli yanayojulikana kama Tour de France.kwa mara nyingine yamekumbwa na kashfa baada ya mwanamichezo wa Ujerumani Patrik Sinkewitz kugundulika kuwa ametumia madawa ya kuongeza nguvu. Kutokana na hayo mashirika ya serikali ya televisheni ya ARD na ZDF yameamua kuacha kuyatangaza mashindano hayo moja kwa moja.


Gazeti la HANDELSBLATT kutoka mji wa DÜSSELDORF, linasema kuwa athari za kashfa hiyo hazitaishia tu katika uamuzi wa mashirika hayo ya televisheni kusimamisha matangazo ya moja kwa moja. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa hata wadhamini wa mashindano hayo na hasa wa shirika la Telekom, wangelifanya jambo la busara kujitenga na mashindano hayo ya kashfa.Mhariri huyo anasema, wenye makampuni hayo wanajua kuwa kuharibika jina la kampuni kunaweza kusababisha hasara kubwa.

Na mhariri wa gazeti la ESSLINGER anaunga mkono mtazamo huo kwa kusema lingekuwa jambo la busara kwa wadhamini kujitenga na mashindano hayo.Anasema mashindano hayo ya mbio za baiskeli Tour de France , sasa hayafai tena, kutumika kama mfano bora kwa vijana.

Na gazeti la RHEIN- NECKAR- ZEITUNG linasema katika maoni yake kwamba mambo sasa yamegeuka kwa wadanganyifu. Televesheni haitatangaza tena udanganyifu huo , wadhamini pamoja na waajiri watatoeka.


Katika maoni yao wahariri leo pia wanazungumzia urari wa kazi iliyotimizwa na kansela wa Ujerumani bibi Angela Merkel tokea aanze kushika wadhifa huo.

Wahariri karibu wote wanampongeza bibi Merkel kwa mafanikio ya hadi sasa.

Kwa mfano gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linasema kuwa hata washindani wake kama Oskar Lafontaine wa chama cha mlengo wa kushoto, wanapaswa kutambua kwamba bibi Angela Merkel anaungwa mkono.

Hatahivyo mhariri wa gazeti la MANNHEIMER MORGEN anatilia maanani kwamba wakati bibi Merkel anang’ara kama Kansela , ngebe zimezidi katika serikali yake ya mseto ya vyama vya CDU na Social Demokratik.

Mhariri wa gazeti la DRESDENER NEUSTEN NACHRICHTEN anaunga mkono maoni hayo kwa kusema kuwa serikali hiyo ya mseto haina matao ya kumwinua mtu kitini.Kwani imecheza ngoma vibaya katika masuala ya mageuzi ya afya, kodi na mshahara wa kima cha chini.

AM.