1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya9 Januari 2014

Wahariri wanatoa maoni juu ya uwezekano wa kuibadilisha ratiba ya fainali za kombe la dunia nchini Qatar na kuhusu aliyoyasema aliekuwa Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates juu ya Rais Obama. .

https://p.dw.com/p/1Anl9
Rais Barack Obama na aliekuwa waziri wake wa ulinzi Robert Gates
Rais Barack Obama na aliekuwa waziri wake wa ulinzi Robert GatesPicha: picture-alliance/dpa

Huenda ratiba ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2022 nchini Qatar ikabadilishwa, kutokana na sababu ya hali ya hewa. Kutokana na joto kali katika nchi hiyo huenda mechi zikachezwa katika msimu wa baridi.

Juu ya uwezekano huo mhariri wa gazeti la "Donaukurier" anasema kwamba tokea mwanzo kabisa lilikuwa kosa kuichagua Qatar kuwa mahala pa kuchezea fainali za kombe la dunia.Mhariri huyo anasema bado palikuwa na muda wa kufanya marekebisho, lakini Rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA,Bwana Blatter hakuwa na kifua cha kuyafanya marekebisho hayo.

Mhariri wa gazeti la "Saarbrücker" anatilia maanani kwamba uwezekano ulioashiriwa na Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke juu ya kuibadilisha ratiba ya mashindano umekanushwa. Mhariri huyo anasema hiyo ni ishara kwamba shirikisho la FIFA, ni kikundi cha mafisadi na litaendelea kuwa hivyo, kama inavyojulikana tokea muda mrefu.

Robert Gates

Aliekuwa Waziri wa ulinzi wa Marekani,Robert Gates amemkosoa vikali Rais Barack Obama juu ya masuala ya ulinzi. Ametoa lawama kali katika kitabu cha kumbumbuku zake.

Mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" anasema mpaka sasa bwana Robert Gates alikuwa anazingatiwa kuwa mtumishi wa kuaminika wa utawala wa Obama. Lakini sasa wakati ambapo amestaafu, waziri huyo wa zamani ameuvunja uaminifu. Katika kitabu cha kumbukumbu zake bwana Gates amemkosoa vikali Rais Obama juu ya sera yake kuhusu Afghanistan.

Mpaka siku ya kumuaga waziri wake, Rais Obama alimsifu sana bwana Gates kwa utiifu wake. Lakini sasa hakuna kilichobakia katika utiifu huo.

Na gazeti la "Tagesspiegel" linauliza katika maoni yake jee aliyofanya Robert Gates ni sahihi kumkosoa Rais Obama baada ya kustaafu? Mhariri wa gazeti hilo analijibu swali lake mwenyewe kwa kueleza kwamba Marekani inalijadili swali muhimu .

Rais Obama aliingia madarakani wakati vita vimeshasonga mbele nchini Afghanistan.Lakini vita hivyo vinaenda kinyume na maadili yake na ndiyo sababu ameamua kuyaondoa majeshi ya Marekani. Obama ameyapitisha maamuzi ya kuhistoria nchini Iraq na Afghanistan. Anachopaswa kukifanya sasa ni kuwaeleza watu wake kwamba yeye hakuyasahihisha tu makosa yaliyofanywa na utawala wa hapo awali bali yeye pia anao uwezo wa kuiongoza Marekani.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef