1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya22 Agosti 2012

Wahariri karibu wote wanaizungumzia kauli aliyoitoa Rais Barack Obama juu ya mgogoro wa Syria.Obama ametoa onyo kwa utawala wa Assad, kwamba Marekani itatumia nguvu za kijeshi ikiwa Assad atazitumia silaha za sumu.

https://p.dw.com/p/15u5c
Rais Barack Obama atoa onyo dhidi ya Assad
Rais Barack Obama atoa onyo dhidi ya AssadPicha: dapd

Juu ya onyo la Obama mhariri wa gazeti la "Die Welt" anasema kauli ya Rais ni huyo ni ishara ya kukubaliana na Israel.Kwani katika miezi iliyopita Israel tayari ilikuwa inafikiria kuishambulia kijeshi Syria ili kuziteketeza silaha za maangamizi za utawala wa Assad.

Na mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anatahadharisha kwamba mgogoro wa Syria utaingia katika hatua mbaya ikiwa utawala wa Assad utazitumia silaha za sumu. Mhariri huyo anasema mgogoro wa Syria utaingia katika hatua ya hatari kubwa ikiwa silaha za sumu zitatumiwa na utawala wa Assad .Lakini hatari hiyo haitakuwa tofauti , ikiwa silaha hizo zitaingia katika mikono isiyostahili.Mikono hiyo isiyostahili, inaweza kuwa Hezbollah, au Iran au waislamu wenye itikadi kali. Madhara yake kwa nchi za jirani yatakuwa makubwa,kiasi kwamba yanayotokea Afghanistan ni mzaha tu.

Gazeti la "Schweriner "linauliza, jee Rais Obama sasa anataka kuonyesha misuli kwa utawala wa Assad.? Mhariri wa gazeti hilo analijibu swali hilo kwa kueleza kwamb hata ile hatua tu, ya kuwaunga mkono wapinzani wa Syria kwa silaha ilikuwa mwiko kwa utawala wa Obama. Hata hivyo Marekani inawaunga mkono wapinzani wa Syria kwa mahitaji mengine, sambamba na kukubaliana na marafiki zake, katika nchi za kiarabu, wanaowapa silaha wapinzani wa Assad. Sera hiyo inathibitisha kwamba,Marekani haina dhamira ya kujiingiza kijeshi, moja moja nchini Syria tofauti na ilivyokuwa nchini Libya. Lakini sera ya Marekani ya kuendelea kujizuia, kwa upande mwingine maana yake ni kuendelea kwa mapigano nchini Syria.

Gazeti la "Der Neue Tag" linatuhumu kwamba Rais Obama anayo malengo mengine anapotoa onyo kwa utawala wa Assad.Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema kuwa Rais Obama anaona kampeni za uchaguzi zimepamba moto nchini Marekani. Washindani wake wa Republican wanalipigia chapuo suala la kile wanachokiita udhaifu wa sera ya nje ya Marekani kutokana na utawala wa Obama, na mapungufu katika mshikamano na mshirika mkuu wa Marekani katika Mashariki ya Kati yaani Israel. Katika kauli yake Rais Obama amechora mstari ,ambao ukivukwa na utawala wa Assad, Marekani itachukua hatua za kijeshi.Lakini Obama ana kigezo gani cha kuupimia mstari huo.?"Tunasema ikiwa utawala wa Assad kwa mara nyingine utatishia kuzitumia silaha za sumu, au ikiwa kutokana na vurumai ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ,udhibiti wa silaha hizo utaenda mrama, Obama atapaswa kuchukua hatua.


Mwandishi:Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen

Mhariri:Josephat Charo