1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI.

Abdu Said Mtullya22 Novemba 2011

Wahariri watoa maoni juu ya Misri.

https://p.dw.com/p/13F10
Mapambano yanaendelea mjini Cairo.Picha: dapd

Wahariri wa magazeti pia wanatoa maoni yao juu ya uchaguzi mkuu nchini Uhispania.

Kuhusu yale yanayotokea sasa nchini Misri gazeti la Mannheimer Morgen linasema utawala wa kijeshi nchini humo unautumia mkono wa chuma kama ulivyofanya utawala wa Mubarak.

Katika maoni yake mhariri wa Mannheimer Morgen ameyakariri madai yaliyotolewa na Shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International kwamba utawala wa kijeshi nchini Misri unazikiuka haki za binadamu kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko utawala wa Mubarak.

Mhariri wa gazeti la Brauschweiger ana wasiwasi kwamba huenda jeshi nchini Misri likachukua hatua, mithili ya zile zilizochukuliwa na jeshi la nchini Uturuki. Mhariri huyo anafafanua kwamba jeshi nchini Misri limeonyesha kwamba halipo tayari kuyakabidhi mamlaka kwa raia. Pana vigezo vya kushangaza vinavyofanana na yaliyotokea nchini Uturuki. Kwa muda wa miaka mingi jeshi liliidhibiti serikali nchini Uturuki na liliwakandamiza wapinzani. Na matokeo yake yalikuwa kuingizwa Uislamu wa kisiasa.

Mhariri wa Sächsiche Zeitung anasema Misri sasa inakabiliwa na kitendawili na anaeleza kuwa katika upande mmoja, ni vigumu kuona jinsi uchaguzi utakavyoweza kufanyika kutokana na mazingira yaliyopo. Lakini katika upande mwingine kuahirisha uchaguzi kutakuwa na maana ya kuwapa ushindi wale wasiotaka kuona mabadikiliko nchini Misri.

Mhariri wa Berliner Morgenpost anasema harakati za mapinduzi zimerudi tena kwenye uwanja wa Tahrir mjini Cairo, baada ya Wamisri kutambua kwamba walibadili mkakasi kwa kichelema!

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo pia wanatoa maoni yao juu ya matokeo ya uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Uhispania ambapo Chama Cha Kisoshalisti kilichokuwa kinatawala kiliangushwa vibaya katika uchaguzi huo. Gazeti la Mitteldeutsche linasema mabadiliko ya uongozi pekee hatayachangia katika kuleta hali nzuri. Umoja wa Ulaya sawa na mabenki hayatampa Waziri Mkuu mtarajiwa, Mariano Rajoy muda wa kuyafafanua mageuzi anayopaswa kuyatekeleza. Hapo jana, tayari riba za madeni ya Uhispania zilipanda katika kiwango ambacho hakuna nchi inayoweza kukimudu. Waziri Mkuu matarajiwa Rajoy hatakuwa na njia nyingine ila kubana matumizi yatakayowaumiza sana watu wake.

Naye mhariri wa Nürnberger Nachrichten analalamika kwamba kwa muda mrefu, kashfa imeruhusiwa kustawi katika Umoja wa Ulaya.Watu Milioni tano, na hasa vijana hawana ajira nchini Uhispania. Kiwango hicho hakina mithili katika Umoja wa Ulaya. Viongozi wa Uhispania waliovimbiwa hawakuyajali hayo. Wameifilisi Uhispania kama jinsi madiketa wa upande mwingine wa bahari ya Mediterania wanavyofanya.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Josephat Charo