1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti

Abdu Said Mtullya20 Mei 2010

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni yao juu ya tamko la serikali lililotolewa bungeni jana na Kansela Merkel.

https://p.dw.com/p/NTB0
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.Picha: dpa

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametahadharisha kwamba sarafu ya Euro imo hatarini.Na ikiwa itaanguka basi Umoja wa Ulaya pia utaanguka.Alisema hayo jana katika tamko la serikali.

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya kauli hiyo.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linasema Kansela Merkel ametoa changamoto kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya.Nchi hizo zinapaswa kufuata njia moja, itakayozielekeza kwenye umoja badala ya kuzingatia maslahi ya kitaifa.

Lakini mhariri wa gazeti la Emder hakubaliani na kauli iliyotolewa na Kansela Merkel kwamba sarafu ya Euro imo hatarini. Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema kwamba wanasiasa wana tabia ya kutumia kauli nzito wanapokusudia kuzipitisha ajenda zao. Bibi Merkel amesema kuwa Umoja wa Ulaya pia umo hatarini na ametahadharisha juu ya uwezekano wa kusambaratika kwa Umoja huo! Mhariri wa gazeti la Emder anasema taswira za aina hiyo ni hatari. Zinaweza kuwaelekeza watu katika njia ambayo hatimaye watashindwa kuidhibiti. Mhariri huyo anakubaliana na Kansela Merkel kwamba Euro imo hatarini, lakini anasema ,haina maana kwamba Umoja wa Ulaya utavunjika.

Gazeti la Fuldaer linapinga hoja,kwamba mgogoro wa Euro umesababishwa na walanguzi. Gazeti hilo linasema picha inayowasilishwa na Kansela Merkel siyo sahihi. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa walanguzi wanatumiwa kama kisingizio cha kutokea kwa mgogoro wa Euro.Lakini gazeti hilo linasema walanguzi hao wanaoitwa nzige siyo chanzo cha matatizo- Gazeti linaeleza kuwa matatizo yanayoikabili sarafu ya Euro,ni matokeo ya kukopa sana ambako kumekuwa kunafanywa na kunakofanywa na serikali kwa muda wa miaka mingi.

Gazeti la Fuldaer linakumbusha kwamba,katika kampeni zao za uchaguzi wanasiasa wa Ulaya wanatoa ahadi za kuwapa wananchi wao maisha mazuri. Lakini mhariri huyo anasema maisha hayo mazuri hayawezi kuletwa bila ya jasho. Lazima kwanza watu wafanye kazi ili kuleta neema.

Katika tamko lake bungeni jana,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia aliwaambia wajerumani,kwamba wao pia wamekuwa wanaishi nje ya uwezo wao. Amesema wajerumani wamekuwa wanaishi kwa kukopa kwa muda wa miaka mingi.Na Sasa umefika wakati wa kuanza, kuwa waangalifu. Lakini gazeti la Bild Zeitung halikubaliani na kauli ya Kansela Merkel.Gazeti hilo linasema siyo wananchi wanaopaswa kuwa waangalifu bali ni serikali.

Na mhariri wa gazeti la Der neue Tag anaongeza kwa kueleza kwamba kwa muda wa miaka mingi serikali za Ujerumani zimekuwa zinakopa na zimeigeuza tabia hiyo kuwa kama hisani kwa wananchi. Gazeti hilo pia linasema siyo mwananchi ambae amekuwa anaishi nje ya uwezo wake ,bali ni serikali.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman