1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya9 Machi 2010

Jee watu waliowatendea watoto uhalifu makanisani waadhibiwe hata baada ya miaka mingi kupita?Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao.

https://p.dw.com/p/MOGx
Kasisi Johannes Bauer anaekabiliwa na tuhuma za kuwanyanyasa watoto kwenye nyumba ya utawa ya Ettal.Picha: AP

Mikasa juu ya kuharibiwa kwa watoto wa kiume na makasisi na watu fulani wengine kwenye taasisi kadhaa za kanisa na elimu imeingia katika hatua mpya nchini Ujerumani.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia hayo katika maoni yao.

Gazeti la Flensburger Tageblatt linasema kurefusha muda kwa miaka 30 au hata miaka 40 ambapo wahalifu wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria baada ya kutenda uhalifu, hakutawasaidia waliotendewa uhalifu. Mhariri anasema kinachoweza kuwasaidia waliotendewa uhalifu ni kurefusha muda wa kupokea pensheni na fidia. Mhariri anatilia maanani kwamba baada ya miaka mitatu watu hao wanapoteza haki ya kupata malipo hayo.

Gazeti la Der neue Tag linasema tatizo juu ya mikasa inayohusu kudhalilishwa kwa watoto wa kiume makanisani ni siyo lini, waliotenda uhalifu wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa tatizo ni ukimya wa muda mrefu baada ya kutendeka kwa uhalifu.

Kufichuka sasa kwa habari juu ya yaliyotokea , kunatia uchungu moyoni.Gazeti linasema habari hizo zimeondoa kabisa imani na zimevuruga uhusiano.

Hatahivyo, mhariri anatumai kwamba maumivu yaliyotokea yatatibika, na hivyo kuwa msingi wa uhusiano mpya baina ya watoto, wazazi na walimu.

Na mhariri wa gazeti la Wetzlarer anasema kurefushwa muda ambapo wahalifu wanaweza kuchukuliwa hatua hakutawaondolea maumivu waliotendewa uhalifu,lakini kutawapa watu uhakika kwamba jamii inawajali. Pamoja na hayo itawaepushia hisia za kuvunjika moyo kwamba watu waliowatendea uhalifu hawapewi adhabu.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung anasema ni vigumu kupima; kipi ni kizito zaidi ,kati ya ukimya wa miaka mingi uliowezesha kutendeka kwa uhalifu, na kupotea kwa imani. Mhariri huyo anasema sasa umefika wakati kwa kanisa katoliki kuchukua hatua ili kurejesha imani hiyo. Na Baba mtakatifu Benedikt wa 16 ndiye mwenye uwezo wa kuongoza mchakato huo. Lakini gazeti la Landeszeitung, linasema ,kwa bahati mbaya hadi sasa zinasikika tu, kauli zinazoashiria kusikitishwa kwa kanisa, kwa jumla juu ya maovu yaliyotokea , lakini hazijasikika kauli kutoka kwa Baba mtakatifu mwenyewe juu ya kutaka wahalifu wachukuliwe hatua.

Hatahivyo, mhariri wa gazeti hilo anasema ni jambo la kutia moyo kwamba Baraza la Maaskofu la Ujerumani limesema kuwa lipo tayari kushiriki kwenye meza ya mazungumzo.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Miraji Othman