1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya5 Januari 2010

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatahadharisha juu ya hatari ya kufanya makosa nchini Yemen kama yaliyofanywa na nchi za magharibi nchini Irak na Afghanistan.

https://p.dw.com/p/LLaT
Rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh.Picha: picture-alliance/ dpa

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya hali ya nchini Yemen,mtanziko unaomkabili rais Obama katika harakati za kupambana na ugaidi duniani na juu ya jengo la mita 800 katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Juu ya hali ya Yemen, Gazeti la Nürnberger Nachrichten linasema makosa yale yale yanaendelea kufanyika kana kwamba hakuna mifano ya kutosha duniani.

Mhariri wa gazeti hilo anazungumzia juu ya hatua za kijeshi ambazo nchi za magharibi zinakusudia kuchukua ili kukabiiliana na tishio la Al-Kaida nchini humo .Mhariri huyo anaeleza kuwa hali ya Yemen inathibitisha kazi ya bure inayofanywa na askari wanapojaribu kuishikilia nchi inayosambaratika.

Gazeti la Nürnberger Nachrichten linasema hali ya Yemen inaonyesha udhaifu wa sera za usalama za nchi za magharibi, kama jinsi ilivyothibitika, Afghanistan,Pakistan na nchini Somalia, yaani zizi la tatu kwa ukubwa duniani katika kuzalishia magaidi.

Gazeti la Reutlinger Anzeiger pia linazungumzia juu ya suala la ugaidi kwa kusisitiza kwamba Marekani na nchi inayofungamana nazo sasa zimesimama njia panda.Gazeti hilo linasema mkakati wa hadi sasa ni wa hasara kubwa na wala haujaleta ufanisi katika harakati za kupambana na ugaidi nchini Afghnaistan na Irak.Mhariri wa Reutlinger Anzeiger anasema na sasa pana uwezekano wa kuanzishwa uwanja mwingine wa mapambano nchini Yemen.Mhariri huyo anasema mtanziko unaomkabili rais Obama unakumbusha hali iliyomkabili rais J. F. Kennedy wakati wa mgogoro wa Cuba. Siyo kwamba mambo yalimzidi kimo tu , bali pia Kennedy alishindwa kuzuia kuendelea kuzama kwa Marekani katika vita vya Vietnam.

Gazeti la Rhein-Zeitung linawakosoa wale waliotoa kauli za kumshambulia Askofu Margot Käßmann aliehoji kwamba kuwepo kwa majeshi ya nje nchini Afghanistan hakujaleta amani katika nchi hiyo.Gazeti linaeleza kuwa Askofu huyo mwanamke hakusema jambo linalokingamana na maadili ya amani ya dini ya kikristo. Mhariri wa gazeti la Rhein-Zeitung, anaeleza kuwa Askofu huyo ana haki ya kuwakilisha msimamo huo. Hata hivyo, gazeti lnasema kuwa, siyo kazi ya kanisa kuiambia serikali nini cha kufanya.Lakini ,gazeti linasema wale wanaounga mkono matumizi ya nguvu za kijeshi nchini Aghanistan, hawana hoja za kukanusha aliyosema Askofu huyo wa Ujerumani.

Gazeti la Neu Westfälische linatoa maoni juu ya jengo refu kuliko lingine lolote duniani,katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mhariri wa gazeti hilo anasema wapinzani wa jengo hilo lenye urefu wa mita 800 wanalalamika kwamba halina manufaa ya kiuchumi. Lakini mhariri huyo anauliza, jee ni nani anaejali hayo katika nchi ambapo kila mwananchi, anatumia wastani wa lita 550 za maji kwa siku? Gazeti linasema yumkini hakuna mwanadamu anaejali ujenzi wa mnara huo uliopo Dubai-lakini anakumbusha kwamba mwenyezi Mungu anaweza kukasirika tena kama alivyokasirika katika enzi za Babilonia.

Gazeti linasema binadamu amekuwa anamkasirisha Mungu kwa muda mrefu, katika Dubai na kwengineko!

Mwandishi/Mtullya abdu Deutcshe Zeitungen.

Mhariri Miraji Othman