1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti walaani adhabu ya kifo!

Abdu Said Mtullya30 Desemba 2009

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanashutumu adhabu ya kifo iliyotolewa na China kwa raia wa Uingereza.

https://p.dw.com/p/LHA1
Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ameishutumu China kwa kutoa adhabu ya kifo kwa raia wa Uingereza.Picha: AP

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya adhabu ya kifo iliyotolewa kwa raia wa Uingereza nchini China.

Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu pendekezo la kutumiwa mashine zinazoweza kuonyesha pia sehemu za siri za mwanadamu wakati wa kudhibiti usalama kwenye viwanja vya ndege.

Adhabu ya kifo iliyotolewa kwa raia wa Uingereza Akmil Shaikh ilitekelezwa hapo jana nchini China. Juu ya adhabu hiyo gazeti la Bild- Zeitung linasema katika maoni yake, kwamba kwa mara nyingine China imeonyesha tabia ya kikatili.Lakini mhariri huyo pia anasikitika kuwa malalamiko dhidi ya adhabu hiyo yanatolewa kwa sauti za chini.Anaeleza kuwa sababu ya mtazamo huo ni kwamba hakuna anaetaka kukwaruzana na China kutokana na umuhimu wake wa kibiashara.

Gazeti linasema kibiashara China ni mteja mkuu wa nchi za magharibi na nchi hiyo inatarajiwa kushika nafasi ya kwanza duniani, katika kuuza bidhaa nje. Lakini gazeti la Bild -Zeitung linatanabahisha juu ya kukiukwa kwa haki za binadamu nchini China.Mhariri anasema, kwa wastani watu mia moja wananyongwa nchini humo kila siku.

Gazeti hilo linazitaka nchi za magharibi kutokubali asilani ukiukaji wa haki za binadamu nchini China. Gazeti linasema China inahitaji kupewa somo juu ya demokrasia.Na njia ya kufikia lengo hilo ni kuibana ,kisiasa na kiuchumi.

Gazeti la Braunschweiger linatilia maanani fimbo inayotumiwa na China katika uhusiano wake na nchi nyingine.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa siku zote China inazionya nchi nyingine juu ya uwezekano wa kuvurugika kwa uhusiano, nchi hizo zinapoilaumu kuhusiana na haki za binadamu. Gazeti linatoa mfano wa adhabu kali ya kifungo jela, iliyotolewa kwa mwaharakati wa haki za binadamu Liu Xiaobo.

Kutokana na kukiukwa kwa haki za binadamu nchini China, gazeti la Braunschweiger linasema ni kichekesho kikubwa ,kwa wataalamu wa nchi za magharibi kuizungumzia China kuwa ni nchi inyoinukia kuwa dola kuu jipya duniani.

Lakini gazeti la Der neue Tag linawakumbusha viongozi wa nchi za magharibi kwamba, adhabu ya kifo haitolewi nchini China tu!Kwa mfano, gazeti hilo linamkumbusha waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, kwamba adhabu ya kifo inatolewa hata na rafiki zake wa Marekani, watawala wa Pakistan na Saudi Arabia. Gazeti hilo linasisitiza kwamba katika nchi hizo adhabu ya kifo pia imeidhinishwa na serikali.

Baada ya mkasa wa mwananchi wa Nigeria alieweza kuingia katika ndege na milipuko, sasa pana pendekezo juu ya kuanza kutumia mashine za mmuriko zinazoweza kuonyesha hata sehemu za siri za mwanadamu ,lakini kwa manufaa ya usalama wa abiria.

Juu ya pendekezo hilo gazeti la Rhein Zeitung linakumbusha kwamba mashine hizo zilipingwa hapo awali ati kwa sababu ya uwezekano wa kukiukwa hadhi ya mwanadamu. Katika udhibiti wa usalama mashine hizo pia zinaweza kuonyesha sehemu za siri za mwanadamu.

Lakini gazeti hilo linasema, laiti mashine hizo zingelitumika, gaidi kutoka Nigeria asingeliweza kuingia ndani ya ndege na vitu hatari!

Mwandishi/ Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.

Mhariri/ Miraji Othman