1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya30 Septemba 2009

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya mabadiliko ya uongozi yanayofanyika katika chama cha Social Demokratik-SPD

https://p.dw.com/p/JuS2
Guido Westerwelle anaetarajiwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani.Picha: AP

Chama cha Social Demokratik kinafanya mabadiliko makubwa katika uongozi wake kufuatia kushindwa kwake vibaya katika uchaguzi mkuu hapa nchini .Hilo ndilo suala linalozingatiwa leo na wahariri wa magazeti , kwa mapana na marefu.


Katika maoni yao wahariri hao pia wanazumngumzia atakaekuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Bwana Guido Westerwelle ambae ni shoga.

Gazeti la Berliner Post linatoa maoni juu ya mabadiliko ya uongozi katika chama cha social demekratik SPD kufuatia kushindwa vibaya sana katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Ujerumani jumapili iliyopita.

Gazeti hilo linasema chama cha SPD kinahitaji kuwa na mtu wa haiba ya Gerhard Schröder, lakini awe Schröder wa kisasa. Yaani mtu mwenye uwezo wa kuileta pamoja mirengo yote ya chama. Mhariri wa Berliner Post anasema chama cha SPD kinamhitaji mtu mwenye uwezo wa kuleta maridhiano baina ya watetezi wa mrengo wa shoto na mrengo wa kati katika chama- lakini mtu huyo awe mwanasiasa anaepigania mfumo wa mishahara ya kima cha chini na anaeunga mkono kodi za biashara za chini.

Gazeti la Nordwest-Zeitung pia linasema chama cha SPD lazima kifanye mabadiliko katika uongozi ikiwa kinataka kuendelea kuwa hai.

Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba pana mvutano baina ya wanachama wa mrengo wa shoto na wa mrengo wa kati. Lakini gazeti linasema chama cha SPD lazima pia kibadili maudhui ya programu yake ili kuepusha uongozi kuchukuliwa na wanaitikadi kali wa mrengo wa shoto.


Gazeti la Frankfurter Neue Presse linazungumzia mpangilio wa uongozi mpya unaotarajiwa katika chama cha wasocial democrats na linasisitiza kuwa ,ikiwa chama cha SPD kinataka kuendelea kuwa hai ,lazima kirejee katika msimamo wa kutetea haki za kijamii.

Linapozungumzia uongozi mpya gazeti hilo lina maana ya kuwataja Sigmar Gabriel aliekuwa waziri wa ulinzi wa mazingira wa Ujerumani.Sasa anatarajiwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama cha SPD.Gazeti linamsifu bwana Gabriel kuwa mwanasiasa mwenye ulumbi, uwezo wa kujieleza.

Mhariri wa Frankurter Neue Presse anaeleza katika maoni yake, kwamba bwana Sigmar Gabriel na mwenzake Andrea Nahles anaeterajiwa kuwa katibu mkuu,ni jozi itakayotangamana vizuri.

Gazeti hilo linaeleza matumaini kwamba mabadiliko ya uongozi yanayofanyika katika chama cha SPD yatakiwezesha chama hicho kupita katika mtihani mgumu unaokikabili.

Guido Westerwelle.

Gazeti la Express kutoka mjini Kolon leo linamzungumzia Guido Westerwelle anaetarajiwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani.Bwana Westerwelle anahesabika kuwa mshindi mkubwa wa uchaguzi na chama chake cha waliberali FDP, lakini gazeti la Express linatilia maanani kwamba Westerwelle atakuwa waziri wa mambo ya nje wa kwanza wa Ujerumani ambae ni shoga. Watu wanauliza hiyo itawezekana vipi?

Lakini gazeti la Express linasema ushoga wake hauna uhusiano na uanasiasa wake. Na mbali na hayo gazeti linatamka ,Ujerumani ina haki ya kumpa jukumu yeyote kuiwakilisha katika nchi za nje.

Mwandishi Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.

Mhariri/Abdul-Rahman