1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Charo, Josephat14 Julai 2008

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia kuundwa kwa muungano wa nchi za Mediterenia katika mkutano uliofanyika mjini Paris Ufaransa na sera za serikali ya Ujerumani kuhusu kodi.

https://p.dw.com/p/Ec9D
Rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: AP

Tunaanza na kuundwa kwa muungano wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia. Gazeti la Ostsee Zeitung la mjini Rostock linampongeza sana rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy.

Mhariri anasema rais Sarkozy ameuwasilisha uongozi wa kisiasa wa nchi za kusini mwa bahari ya Mediterenia na viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya kwenye meza ili kuusalimisha mradi wake wa kuundwa kwa umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia. Muungano huo unalenga kusaidia kuimarisha kazi ya pamoja inayofanywa kwenye mipaka ya bahari hiyo.

Gazeti la Ostsee Zeitung linasema rais Sarkozy akiwa kama rubani wa meli ya Ulaya sasa ameweka kasi mpya ya safari. Nchi za kaskazini na kusini mwa bahari ya Mediterenia zinarudiana karibu. Bila shaka katika maswala ya kisiasa bado kila kitu kinabakia kwenye makaratasi tu, lakini mradi huu wa kuundwa kwa umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia ni juhudi inayofaa kupongezwa.

Nalo gazeti la Frankfurter Rundschau lina maoni haya: Ufanisi wa Umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia utapimwa kulingana na umbali utakaoweza kuondoa mapungufu ya mkataba wa Barcelona na ikiwa utakuwa umeunda mkakati wa kisiasa unaoenda sambama na masilahi ya Umoja wa Ulaya. La muhimu litakuwa vipi nchi za kusini mwa bahari ya Mediterenia zitakavyokuwa na maingiliano.

Viongozi wa nchi 16 za kusini mwa bahari ya Mediterenia walihudhuria mkutano wa mjini Paris Ufaransa, lakini rais wa Libya, Muamar Gaddafi hakuhudhuria. Syria na Libanon zinataka kwa mara nyingine tena kuwa na uhusiano wa kibalozi. Naye waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa mamlaka ya Wapalestina, Mahmud Abbas, waliweka mikoni yao kwenye mikono ya mwenyeji wa mkutano wa Paris, rais Nicholas Sarkozy.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Rundschau anasema hayo yote kwanza yana maana ya kihistoria tu.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung katika maoni yake linasema kuundwa kwa muungano wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia hakujatoa hisia za ufanisi mkubwa wa kihistoria kama rais Sarkozy alivyofikiria.

Mhariri anasema ni mapema mno kuwepo kwa muungano halisi kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati. Hakujakuwepo na uaminifu wa kutosha miongoni mwa nchi hizo. Historia inadhihirisha kumekuwepo na nyakati nyingi za kuvunja moyo kuliko ufanisi.

Mada nyengine iliyowashughulisha wahariri leo ni sera za kodi za serikali ya Ujerumani. Gazeti la Die Welt likizingatia kupanda kwa bei ya nishati linasema swala la jinsi ya kukabailiana na kupanda kwa bei za nishati linategemea maelewano msingi kuhusu sera za kodi.

Mhariri wa Die Welt anauliza je wanasiasa wa Ujerumani wanatakiwa kwa umbali gani waongeze juhudi zao kufahamu hisia za wananchi? Je wanatakiwa wawape bia za bure wapigaji kura wakati wanapokuwa na kiu? Au wanatakiwa waunde malengo ya muda mrefu ambayo wanatakiwa kuyafikia licha ya kuwepo upinzani?

Mhariri wa gazeti la Die Welt anasema kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameamua kutozipa kipaumbele sera kuhusu kodi na fedha na ameamua kuliweka mwisho swala hili. Mhariri anasema, hili sharti litambulike wakati huu.