1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Charo19 Desemba 2007

Wahariri wanazungumzia matamshi ya rais Fidel Castro kuwa hatawazuia vijana kuitawala Cuba

https://p.dw.com/p/CdaL
Rais Fidel Castro (kushoto)na kakake Raul CastroPicha: AP

Rais wa Cuba, Fidel Castro ametawala kwa kipindi kirefu kuliko muda wa utawala wa kisoshalisiti wa Ujerumani Mashariki, DDR. Kukubali kwake juu ya uwezekano wa kuachia madaraka kumezusha wimbi kubwa la hisia mbalimbali katika ngazi ya kimataifa na hata wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani leo hawakuwa na budi kutoa maoni yao na kuchambua kauli hiyo ya rais Fidel Castro. Aliyeyakusanya maoni ya wahariri leo ni Josephat Charo.

Gazeti la Ostsee Zeitung la mjini Rostock ambalo kwanza linajaribu kutoa picha halisi. Mhariri anaanza kwa kusema Adios Fidel, kwaheri Fidel, au bado muda haujafika? Bila shaka rais Fidel Castro ataaga kwa kutoa wasia. Swali kubwa linalojitokeza hata hivyo si lini mwanasiasa huyo wa kisoshalisti atakapong´atuka madarakani, ila vipi Cuba itakavyoendelea mbele bila yeye. Mrithi wake, kakake Raul Castro, ambaye tayari ana umri wa miaka 76, bado hajaamua kati ya utawala wa mkono wa chuma na kufungua uhusiano wa kidiplomasia kwa uangalifu mkubwa.

Juhudi za kuleta mageuzi katika kisiwa cha Cuba ambayo yanahitajika mno na wananchi wa nchi hiyo, na pia hatimaye yanayoweza kuubadili msimamo wa hasimu wake Marekani, ni nadra sana kuonekana. Pia kwa sababu rais Fidel Castro na viongozi wake serikalini wana matumaini kwamba usoshalisti nchini Cuba utaendelea kubakia katika hali nzuri milele kupitia jua, samba na kitita cha mafuta kutoka kwa dikteta wa Venezeula, rais Hugo Chavez, ambaye leo hii anatarajiwa kula chakula cha mchana na rais Fidel Castro mjini Havana.

Rais Fidel Castro anaipa nafasi Cuba, limeandika gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin katika kichwa chake cha habari. Pekee ukweli kwamba nchini Cuba kwa kipindi cha karibu miaka 20 tangu kumalizika mfumo wa usoshalisti halisi bado mpaka sasa mfumo huo unaendelezwa. Ukweli ni kwamba kwa hali ya baadaye ya jamii ya Wacuba ni huzuni. Cuba inakabiliwa na shinikizo kubwa la ndani ya nchi kuliko shinikizo kutoka nje. Tayari raia wa Cuba walio na elimu nzuri na wanaojivunia mapinduzi, hukihama kisiwa cha Cuba kwa idadi kubwa kwa sababu nchi yao haiwapi mwelekeo mzuri.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung la mjini Munich linaangazia msimamo wa nchi za magharibi kuhusu usoshalisti wa kisiwa cha Cuba.

Mhariri anasema rais Fidel Castro ameshawahi kusema mara moja kwamba historia itazungumzwa kwa uwazi. Hali ya sasa inazusha mjadala wa hali ya wasiwasi nchini Cuba. Mpasuko katika serikali ya mseto ya Ujeruamni mjini Berlin unazidi kwa sababu kuna kambi za zamani serikalini. Chama cha Christian Democratic Union, CDU, kinataka kufuata ukaidi wa Marekani. Hilo halina gharama yoyote kwa sababu Cuba si muhimu sana kama vile China ambako mikataba ni muhimu zaidi kuliko haki za binadamu.

Sehemu ya chama cha Social Democratic, SPD, inaunga mkono kuikaripia Cuba. Na chama cha Christian Social Union, CSU cha Bayern tayari kimekuwa kikifanya biashara na Cuba. Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung anamalizia kwa kusema huu ni wakati wa kufanya mdahalo wa maana na Cuba, iwe rais Fidel Castro atakuwepo au asiwepo.

Gazeti la Neues Deutschland linaloegemea sana chama cha upinzani cha PDS, linajaribu kuzieleza taarifa kutoka mjini Havana kuwa za kawaida. Mhariri anasema Wacuba watalipa kutokana na utulivu wao. Fidel Castro hataki tena kuachana na uongozi wa vyombo vya serikali. Akiwa na umri wa miaka 81 anakaribia kustaafu rasmi lakini bado atakuwa na mamlaka makubwa na atakuwa mshauri mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa.

Ukweli ulio wazi ni kwamba rais Fidel Castro hataki kustaafu, kama inavyotakikana baada ya uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Januari. Ni bahati tu kwamba sasa Castro hatawazuia vijana wanaoweza kuiongoza Cuba hata ingawa bado kuna changamoto nyingi nchini humo.