Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo | Magazetini | DW | 20.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Wahariri wamegusia mzozo wa mashariki ya kati na uamuzi wa serikali ya Ujerumani kuhusu kiwango cha chini cha mshahara kinachotakiwa kulipwa wafanyakazi hapa nchini.

Tukianza na mzozo wa mashariki ya kati, gazeti la Lautsitzer Rundschau la mjini Cottbus limesema hali ya kisiasa ya Mashariki ya Kati imebadilika ghafla. Ndoto ya kuwa na taifa huru la Wapalestina haipo tena bali sasa kuna maeneo mawili, moja la Ukanda wa Gaza likitawaliwa na chama cha Hamas na eneo la Ukingo wa magharibi wa mto Jordan linalotawaliwa na chama cha Fatah.

Mhariri amesema kwa mujibu wa mpango wa sasa wa kutafuta amani baina ya Israel na Palestina lengo lilikuwa hatimaye kuwa na mataifa mawili kwa makabila mawili, yaani taifa la Waisraeli na Wapalestina ambao wangekaa na kuishi pamoja kwa amani.

Lakini sasa ukweli uliopo ni kwamba kuna mataifa matatu kwa makabila mawili. Ukanda wa Gaza unaotawaliwa na Wapaletina wafuasi wa chama cha Hamas, Ukingo wa magharibi wa mto Jordan unaotawaliwa na Wapalestina wafuasi wa chama cha Fatah na taifa la Israel.

Nalo gazeti la Oldenburgische Volkszeitung la mjini Vechta limesema kugawanywa kwa maeneo ya Wapalestina kuna maana matumani ya kupatikana amani baina ya Wapalestina na Waisraeli yamepata pigo kubwa.

Hatua ya jumuiya ya kimataifa kujitolea kwa dhati kumsadia rais Mahmoud Abbas wa mamlaka ya Paletina na chama chake cha Fatah ina maana amani baina ya Israel na sehemu hii ya Wapalestina huenda hatimaye ikafikiwa.

Lakini katika Ukanda wa Gaza jumuiya ya kimataifa inaweza kusahau kuhusu amani baina ya Wapalestina wa eneo hilo na Waisraeli. Mhariri anamalizia kwa kusema Marekani inatakiwa ifahamu kwamba mazungumzo yanahitaji muda ili kuutanzua mzozo wa mashariki ya kati na wala sio kulazimisha mambo.

Swala lengine lililowashuhulisha wahariri ni mazungumzo ya serikali ya Ujerumani na uamauzi wake kuhusu malipo ya chini yanayotakiwa kulipwa wafanyakazi hapa nchini. Gazeti la Badische Tagblatt limesema serikali ya mseto ya vyama vya CDU-CSU na SPD hatimaye imefikia makubaliano, ambayo ni kushindwa kwa Franz Munterfering na wenzake wa chama cha SPD.

Makubaliano hayo yanalenga kuongeza kiwango cha mshahara wa chini unaotakiwa kulipwa wafanyakazi wa Ujerumani, hatua ambayo ni ushindi kwa chama cha CDU-CSU cha Bi Angela Merkel ambacho kitajipatia sifa kutokana na uamuzi huo. Sera hiyo mpya inawalazimisha waajiri na viongozi wa vyama vya wafanyakazi waweke kiwango maalumu cha malipo ya chini.

Mhariri wa gazeti la Süddeutsche amesema pande zote husika zinatakiwa zifahamu kwamba makubaliano yao hayataweza kamwe kutekelezwa kwa sababu za kiuchumi na hali katika soko la ajira.

Likitukamilishia maoni ya wahariri hii leo gazeti la Frankfurter Rundschau limesema mengi hayatarajiwi kutokana na uamuzi huo wa serikali. Hali ya sasa ya kiuchumi hapa Ujerumani inahitaji mawazo mapya. Kwa hiyo serikali inatakiwa ijitihidi kufikiria njia mpya za kuuimarisha uchumi na kama haiwezi basi ijiuzulu.

 • Tarehe 20.06.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHSe
 • Tarehe 20.06.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHSe