1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI WA MAGAZETI JUU YA MGOGORO WA MADENI

Abdu Said Mtullya9 Agosti 2011

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatahadharisha juu ya kufanya kiherehere juu ya mgogoro wa madeni.

https://p.dw.com/p/12DOj
Soko la hisa la Ujerumani DAXPicha: picture alliance/dpa

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo pia wanatoa maoni yao juu ya mgogoro wa fedha unaoikabili dunia.

Gazeti la Osnabrücker linauzingatia mgogoro huo baada ya hotuba ya Rais Obama. Rais huyo alikuwa anazungumzia juu ya tathmini iliyotolewa na Shirika la Standard& Poor's ya kuuteremsha uwezo wa Marekani wa kulipa madeni. Gazeti hilo linasema hotuba ya Obama iliyoonyesha sura ya udhaifu. Mhariri anasema badala ya kuonyesha msimamo wa upambanifu dhidi ya wapinzani wake Obama alitumia maneno ya mzaha.

Gazeti la Neue Osnabrücker limeitilia maanani kauli ya Obama kwamba ,Marekani itaendelea kuwa nchi ya kuaminika, hata ikiwa Shirika la kupima uwezo wa nchi wa kulipa madeni linauteremsha uwezo wake.

Mhariri wa gazeti hilo anasema kauli kama hiyo inawaliwaza wananchi wake walioisikia hukumu iliyotolewa na Shirika la Standard & Poor's. Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung anazungumzia juu ya uwezekano wa kurejea mgogoro mwingine wa uchumi nchini Marekani na duniani kote. Anaeleza kuwa, Marekani haina uwezekano wa kuiepusha hali hiyo kutokana na deni lake kubwa. Hali kama hiyo pia inazikabili nchi kadhaa za bara la Ulaya kama Italia na Ufaransa vile vile.

Pamoja na hayo uchumi wa China umo katika hatari ya kudhoofika. Nchi hizo zote ni washirika wa biashara muhimu wa Ujerumani. Mhariri wa Süddeutsche anasena ikiwa ustawi utakwama katika nchi hizo, utashi wa bidhaa za Ujerumani kama mashine na magari utapungua. Hayo tayari yanaweza kubainika katika hesabu za makampuni makubwa kama Siemens na BMW. Mhariri huyo anaeleza kwamba siyo lazima hali hiyo isababishe msambaratiko kama ule wa mwaka wa 2008 lakini kadri uchumi unavyozidi kunywea vivyo ndivyo mashine viwandani zinavyozidi kuzimwa. Na hayo maana yake ni kupotea nafasi za ajira.

Mhariri wa gazeti la Der neue Tag anatahadharisha juu ya kufanya kiherehere kutokana na yanayotokea kwenye masoko ya hisa. Mhariri huyo anaeleza kwamba siyo lazima kila hisa inapoteleza, wanasiasa wafanye taharuki. Na wala siyo jambo la busara kutoa kauli bila ya nadhari kama alivyofanya Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Bwana Barroso. Mhariri huyo anawashauri viongozi wafanye kazi yao kimya kimya ili kujenga njia ya imani kuelekea katika kuimarisha bajeti. Njia hiyo ingeliyatuliza masoko ya hisa.

Katika maoni yake leo gazeti la Berliner Zeitung linazungumzia ghasia zinazoendelea jijini London na katika vitongoji kadhaa vya jiji hilo. Mhariri huyo anasema umasikini siyo sababu ya kutosha ya kumfanya mtu atende uhalifu. Hata hivyo mhariri huyo anaeleza kwamba kutokana na kuongezeka kwa wasiwasi wa maisha na kutokana na uwezekano wa kupitishwa sera za kubana matumizi kwa kiwango kikubwa, Uingereza sasa inakabiliwa na matokeo ya sera za kufumbia macho matatizo ya muda mrefu.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/- Josephat Charo