1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya wanariadha wadanganyifu na juu ya hukumu ya kesi ya Trayvon Martin

Abdu Said Mtullya16 Julai 2013

Pamoja na masuala mengine wahariri leo wanatoa maoni juu ya kuumbuka kwa Tyson Gay na Asafa Powell. Lakini wahariri wanasema wanamichezo wanashinikizwa kukimbia kasi zaidi na kuruka juu zaidi

https://p.dw.com/p/198GZ
Tyson Gay akiri matumizi ya dawa za kuongeza nguvu
Tyson Gay akiri matumizi ya dawa za kuongeza nguvuPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Sächsiche" linaanza kwa maoni juu ya uchumi wa China.

Ustawi wa uchumi wa China umepungua na kubakia katika kiwango cha asilimia 7.5. Waziri Mkuu wa China amesema hakuna haja ya kuwapo wasi wasi na kwamba kiwango hicho cha ustawi ni katika jumla ya mikakati ya China, ikiwa ni kupunguza mkazo wa kuuza nje, ili kulistawisha soko la ndani.

Mhariri wa gazeti la "Sächsische" anasema katika maoni yake kwamba mkakati huo utakuwa na manufaa kwa Ujerumani. Ameeleza, ikiwa sekta ya kati itaimarishwa nchini China, fursa ya viwanda vya Ulaya kuingia katika soko la China pia itakuwa kubwa.

Aliemuua Trayvon Martin hana hatia:

Gazeti la "Sttugarter" linatoa maoni juu ya hukumu iliyotolewa kwa mtu aliemuua mtoto mweusi nchini Marekani, Trayvon Martin. Mtu huyo hakupatikana na hatia ya kumuua mtoto huyo. Gazeti hilo linasema hukumu hiyo inawarudisha watu katika hisia za zamani sana, kwamba, mtu mweusi yumo katika daraja la pili katika jamii ya Marekani. Hata ikiwa Rais wa nchi hiyo sasa ni mtu mweusi.

Panazuka mazingira ambapo,makovu yanafunuka pale ambapo watu walifiriki yalikuwa yameshatibika. Zimmermann aliemuua kijana huyo mweusi, ndiye alieyafunua majeraha .Hasira zimejaa katika vifua vya watu weusi, mithili ya pipa la baruti likisubiri cheche. Hukumu iliyotolewa na mahakama ya kutomwona Zimmerman na hatia ya kumuua Trayvon Martin imewasha baruti miongoni mwa watu weusi nchini Marekani.

Wanamichezo wadanganyifu:

Kulikoni,Tayson Gay na Asafa Powell?Wanariadha hao mashuhuri wa mbio za mita mia moja wameumbuka baada ya kufichuka kwamba wamekuwa wanatumia dawa za kuongeza nguvu. Mhariri wa gazeti la "Landeszeitung "anatoa maoni yake juu ya mkasa huo : anasema kufichuka kwa habari hizo kumewakasirisha mashabiki wa michezo. Sasa kwa mara nyingine wanamichezo wote watatolewa hukumu za hasira na mashabiki wao.Matumizi ya dawa za kuongeza nguvu yametekwa nyara na wanamichezo.

Wanamichezo wanaotumia dawa za kuongeza nguvu wanautumia vibaya umaarufu wao.Watu wanataka adhabu kali zitolewe kwa wanamichezo wadanganyifu.Lakini swali ni iwapo adhabu hizo zitasaidia.Lakini jambo moja linapaswa kutiliwa maanani. Sisi sote,vyombo vya habari,mashabiki wa michezo na wafadhili tunataka kuwaona wanariadha wakikimbia kasi zaidi, na wakiruka juu zaidi. Tunataka kuona viwango vinavyovuka uwezo wa bin-adam.Hayo yanasababisha mashinikizo kwa wanamichezo na makocha wao.

Gazeti la "Landeszeitung" linasema ikiwa mwanamichezo anashindwa kufikia viwango vya kusisimua kwa kutumia nguvu asilia,ni wazi atatumia njia nyingine. Watu hao hawapo peke yao hatiani.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman