1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump anawakilisha mashaka

Admin.WagnerD21 Julai 2016

Wahariri wanatoa maoni juu ya kuteuliwa kwa Donald Trump kuwa mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani na juu ya uhusiano wa Ujerumani na Uingereza.

https://p.dw.com/p/1JT5v
Theresa May akutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Theresa May akutana na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Mhariri wa gazeti la "Neue Westfälische" anamwita Donald Trump kuwa ni mwongo mzoefu, mbaguzi na mtu mwenye chuki. Gazeti hilo linasema kwa kumchagua Trump kuwa mgombea ,chama cha Republican kimejizika chenyewe kisiasa nchini Marekani.

Mhariri wa gazeti la "Rhein" anakumbusha kwamba wagombea urais wanaofanikiwa nchini Marekani,hutoa ahadi nyingi za kuwapa watu matumaini. Lakini kuhusu Donald Trump mambo ni mengine.

Mhariri huyo anaeleza kuwa Donald Trump si mjumbe wa kawaida kwa sababu yeye ni mtu anaewakilisha mtamauko na anapandikiza mbegu za chuki. Na ndiyo sababu ,kwamba kuchaguliwa kwake kuwa mgombea urais ni mbiu ya mgambo ya kutufanya tujihadhari.

Marekani inaihitaji dunia

Mhariri wa gazeti la "Darmstädter Echo" anatafautisha kati ya Donald Trump na mgombea urais wa chama cha Demokrats , Hillary Clinton kwa kusema kwamba angalau mgombea urais huyo anajua kwamba Marekani inaihitaji dunia, na dunia pia inaihitaji Marekani.

Gazeti la " Allgemeine" linazungumia juu ya uhusiano wa Ujerumani na Uingereza baada ya watu wa nchi hiyo kuamua kujiondoa Umoja wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba licha ya Waingereza kuamua kujiondoa, Umoja wa Ulaya na licha ya kuwepo wanasiasa machachari kama vile waziri wa mambo ya nje mpya wa nchi hiyo Boris Johnson, uhusiano baina ya Ujerumani na Uingereza utaendelea kuwa wa mzuri.

Theresa May na Angela Merkel mjini Berlin
Theresa May na Angela Merkel mjini BerlinPicha: Reuters/S. Loos

Hata hivyo mhariri wa gazeti la "Allgemeine" anakiri kwamba hatua iliyochukuliwa na Waingereza ya kujiweka kando ya Umoja wa Ulaya italeta madhara nchini Uingereza na katika Umoja wa Ulaya. Mhariri huyo anasema katika kipindi cha muda mrefu, hakuna upande utakaoibuka na ushindi.

Gazeti la "Allgemeine" linasema ikiwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Theresa May atafanikiwa kuyakabili madhara hayo kwa ustadi, kama jinsi inavyoonekana sasa, jina lake litaingia katika vitabu vya historia lakini akishindwa, ni yeye mwenyewe atakaekuwa historia, yaani ataingia kapuni.

Mhariri wa gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" anautilia maanani uamuzi wa Uingereza wa kusamehe uenyekiti wa muda kwenye Umoja wa Ulaya.Mhariri huyo anasema huo ndiyo mwanzo wa nchi hiyo kuondoka kabisa kutoka kwenye jumuiya hiyo. Hatua inamaanisha kwamba Uingereza inajiweka kando ya shughuli zote za Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen

Mhariri:Caro Robi